Mkurugenzi Songwe agawa pedi sekondari, ahamasisha uandikishaji watoto shuleni
4 November 2023, 07:13
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe, amefanya ziara ya kuangalia hali ya uandikishaji wa Wanafunzi wa Elimu ya awali, Darasa la kwanza na Elimu ya watu wazima (MEMKWA) katika Kata za Namkukwe, Manda na Magamba.
Na Josea Sinkala, Songwe
CPA Kavishe ametembelea baadhi ya Shule za msingi katika Kata hizo ikiwemo shule ya Msingi Mheza Kata ya Namkukwe ambapo amefanikiwa kugawa juisi kwa watoto wote wa elimu ya awali lengo likiwa kuwahamasisha kupenda shule, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya tarehe yake ya kuzaliwa.
“Nimepata wasaa wa kukata keki na watoto wa awali shule ya msingi Mheza. Wamefurahi sana wanangu, nimewalisha keki watoto wote”, amesema CPA Kavishe mkurugenzi wa Halmashauri ya Songwe.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amewaasa wazazi na walezi ambao watoto wao wamefikisha umri wa kuanza shule kuhakikisha wanatumia muda uliobaki kuwaandikisha watoto hao ili waanze masomo Januari 2024.
Pia, CPA Kavishe amewasisitiza wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kuwaandikisha watoto hao ili nao wapate haki yao ya msingi ya elimu.
Zoezi la uandikishaji wa elimu ya awali, Darasa la kwanza na MEMKWA lilianza rasmi Oktoba 1 mwaka huu na litahitimishwa Disemba 31, 2023.
Pia, CPA Kavishe ametembelea na kuzungumza na wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari ya Maweni Kata ya Mkwajuni ambapo amewashauri namna ya kufikia ndoto zao ikiwa ni pamoja na nidhamu, kujitambua na bidii katika masomo.
Akiwa katika shule hiyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amegawa taulo za kike kwa wanafunzi hao ili kuwasaidia kujisitiri na kuhakikisha hawakosi masomo kwasababu ya kukosa taulo.
Hata hivyo, Kavishe amewaahidi wanafunzi hao kuwa changamoto walizozitaja zimechukuliwa na ili kwenda kufanyiwa kazi.
“Nashukuru nimefanikiwa kuzungumza na wanafunzi wa Maweni Sekondari na kugawa taulo za kike ikiwa ni sehemu ya kusherekea kumbukumbu yangu ya siku ya kuzaliwa. Nimesikiliza changamoto zao na zinaenda kufanyiwa kazi, uongozi ni kuacha alama”, amesema CPA Cesilia Kavishe baada ya kuzungumza na wanafunzi hao.
Nao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maweni wamemshukuru Mkurugenzi huyo kwa kuwatembelea na kuwapa zawadi hizo huku wakimwahidi kuwa watazingatia yote aliyowaasa ikiwemo kusoma kwa bidii.