Bodaboda wengi siku hizi wanapenda mizigo,halafu hamuwi na mzigo mmoja
3 November 2023, 22:21
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe Mhe. Solomon Itunda, ameelekeza kuanzishwa Chama cha maafisa usafirishaji Wilaya ya Songwe ambacho kitahusika na uratibu wa masuala yote yanayohusu madereva wanaotoa huduma za usafiri na usafirishaji huku akiwataka kuzingatia Sheria za Barabarani ili kuepukana na ajali.
Na Hobokela Lwinga
Mkuu wa Wilaya Itunda ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Madereva hao kutoka Kata za Mkwajuni na Saza ambapo lengo lilikuwa kutoa elimu za kupunguza na kutokomeza matukio ya ajali hasa za pikipiki Wilayani Songwe.
Akiwa kwenye kongamano hilo Itunda amewataka madereva bodaboda kutulia na ndoa zao kwa amabo tayari wana familia badala ya kupapalika na wanawakewanaokutana nao njiani akiwaita kwa jina la mizigo.
“Mimi nimeshuhudia kijana wa Bodaboda amebeba abiria akiwa njiani akakutana na mzigo akawa anamuangalia yule dada akageuza hadi shingo baada ya kumpita kama haitoshi akaamua kugeuza pikipiki ikabidi abiria aanze kulalamika maana alikuwa anamtoa hapa (Mkwajuni) kumpeleka Saza kisa mzigo”, amesema Dc Itunda.
Unajua hata kama bora uwe na mzigo mmoja sasa wewe kil mzigo unaopita wa kwako halafu unasema huu mkubwa kuliko ule hivi kweli utapona na magonjwa?”, amehoji Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Solomoni Itunda na kuwataka madereva hao kutulia ili kutimiza ndoto zao.
Pia amekemea tabia za ulevi kwa baadhi ya Madereva Bodaboda na madereva wnegine wanaofanya shughuli za usafirishaji abiria hasa wakiwa kazini jambo linalochochea kasi ya kutokea kwa ajali zisizo za lazima ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kwa kipindi cha hivi karibuni Wilayani Songwe.
“Wewe unaamka asubuhi na mapema saa 12 asubuhi mpaka saa mbili usiku unapata elfu ishirini yako kula elfu kumi, elfu tano ya kuanzia kazi kesho elfu tano tunza sasa wewe unaenda kujonga mizigo mpaka mtaji hapana. Mwenzenu mimi nauchukia umasikini, fanyeni kazi kwa malengo”, amesema Dc Itunda.
Pia, Mhe. Itunda ametoa fedha Sh.laki tano (Tsh. 500,000/=) kutoka katika Ofisi yake ambayo itawezesha mchakato wa usajili wa chama hicho kikundwa na kumtaka Diwani wa Kata ya Mkwajuni Mheshimiwa Shaibath Kapingu kusimamia upatikanaji wa Viongozi wa muda watakaosimamia uanzishwaji Chama hicho.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu ya Songwe bila ajali inawezekana limefanyika katika uwanja wa Mkwajuni ambapo kabla ya kongamano hilo, Mhe. Itunda aliambatana na madereva hao na kufanya maandamano ya bodaboda kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya mpaka kwenye uwanja huo.
Katika kongamano hilo, madereva hao wamepata elimu ya sheria na taratibu za matumizi ya vyombo vya moto na alama za barabarani, ambayo imetolewa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani Wilayani Songwe.
Kongambano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe Mheshimiwa Abrahamu Sambila, Diwani wa Kata ya Mkwajuni Mheshimiwa Shaibath Kapingu, baadhi ya waheshimiwa madiwani na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo, taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi na taasisi za kifedha.
Ikumbukwe kongamano hilo liliitishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songwe kwa ajili ya kujadili namna ya kuzuia ajali Wilayani humo, kongamano lililowakutanisha zaidi ya vijana elfu moja ambao ni madereva wa Bodaboda, Bajaji, Guta, Noah na Tax.