Wachimbaji wadogo wa madini Chunya walia na mercury, wapata ulemavu
30 October 2023, 16:01
Teknolojia ni jambo zuri katika ulimwengu wa sasa lakini hali imekuwa tofauti kwa wachimbaji eneo la Chunya ambapo badala ya furaha imegeuka kilio.
Na Hobokela Lwinga
Wachimbaji wadogo wa madini katika eneo la Itumbi kata ya Matundasi wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameiomba serikali kuwatazama kwa jicho la tatu kwa kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kuwasogezea huduma za afya jirani pamoja na kuwapatia mikopo itakayowawezesha kuendesha shughuli zao za uchimbaji.
Wachimbaji hao wameeleza kilio chao mbele ya Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambaye amefanya ziara ya kikazi katika eneo hilo iliyokuwa na lengo la kutembelea migodi na kuzungumza na wachimbaji wadogo, wauzaji, wanunuzi pamoja na kutatua kero zinazowakabili.
Naye mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM mkoa wa Mbeya Yasin Ngonyani amesema tatizo linalowakabili wachimbaji wadogo katika eneo la Itumbi na maeneo mengine ni suala la mitaji, vitendea kazi kwani kwa sasa bado wanatumia teknolojia ya chini haileti tija kwao na taifa pia.
Akijibia changamoto hizo Waziri mwenye dhamana ya madini Anthony Mavunde amesema kutokana na wachimbaji wengi kuchimba madini kwa kubahatisha kutokana na kukosa taarifa wizara kwa kushirikiana na wataalam wameanza mchakato wa kuboresha taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini ili wananchi wasichimbe madini kwa kubahatisha.