Baraka FM

Ukosefu wa bweni unachochea wanafunzi kupata mimba

26 October 2023, 15:05

Mwonekano wa shule ya sekondari Shisyete Mbeya Dc(picha na Josea Sinkala)

Ni wajibu wa Wananchi, wadau wa maendeleo na Serikali kushirikiana kuhakikisha wanajenga mabweni katika shule zao hasa za vijijini ambazo wengi wa wanafunzi wanatoka mbali na kutembea kwenda mashuleni au kulazimika kupangiwa vyumba vya kuishi (mageto) hali ambayo ni hatarishi kwa watoto kujiingiza katika makundi hatarishi.

Na Josea Sinkala, mbeya.

Shule ya Sekondari Shisyete Kata ya Shizuvi Tarafa ya Isangati Mbeya vijijini inakabiliwa na ukosefu wa mabweni hali inayochagiza kushamiri kwa mimba kwa watoto wakike na utoro kwa watoto wa kiume hivyo kukatisha masomo yao.

Shule ya Sekondari Shisyete huko Shizuvi Umalila haifanyi vizuri kitaaluma ambapo katika kuboresha elimu na kuchochea mwamko kwa watoto Serikali inaendelea kutatua kero zinazoikabili shule hiyo ili kuhakikisha watoto wanasoma licha ya baadhi ya wazazi na walezi kutozingatia umuhimu wa elimu.

Katika kusaidia watoto hao kufikia ndoto zao Shule ya Sekondari Shisyete chini ya Mkuu wake Mwal. Onesmo Mwano imepanga kuanza ujenzi wa bweni la watoto wakike ili kusaidia kuepukana na sishawishi na mimba za mapema kutokana na kutembea umbali mrefu kufuata haki elimu.

Mwalimu Mwano anawaomba wazazi na walezi kushirikiana ili wafanikiwe kujenga jengo la bweni la wasichana kwa kuanza ili kuboresha elimu, kupunguza utoro na mimba za mapema na kuwapa ari watoto kusoma zaidi.

Mkuu wa shule ya Shisyete Onesmo Mwano(picha na Josea Sinkala)
Mkuu wa shule ya Shisyete Onesmo Mwano

Afisa elimu kata ya Shizuvi Mwal. Joeli Munuo, anasema elimu ni msingi wa maendeleo hivyo kwa kuzingatia hilo dhamira yao ni kuona Shule ya upili Shisyete inapata mabweni wakianza na bweni la watoto wakike.

Naye Diwani wa Kata ya Shizuvi Mhe.Noah Mwashibanda amesema ataishawishi Serikali Wilayani Mbeya kuwaunga mkono wananchi kujenga mabweni shuleni hapo ili kuwasaidia watoto hasa wakike ambao kwa mwaka huu tu watoto watatu wamekatisha masomo yao kutokana na ujauzito.

Aidha Diwani Mwashibanda amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini Mhe.Oran Njeza kwa kuchangia Sh.Million moja kwenye uanzaji ujenzi huo ambao msingi tayari umechorwa.

Diwani wa Kata ya Shizuvi Mhe.Noah Mwashibanda(picha na Josea Sinkala)
sauti ya Diwani wa Kata ya Shizuvi Mhe.Noah Mwashibanda

Wazazi na walezi wanaiomba Serikali kuanzia Halmashauri ya Mbeya kuwaunga mkono katika ujenzi wa bweni katika shule hiyo ili kuwanusuru watoto wao na mimba na utoro hivyo kukatishwa ndoto zao kielimu.

Wananchi wakizungumzia athari za ukosefu wa bweni