Mgogoro wa ardhi Mbeya wasababisha mapigano, polisi watumia mabomu
11 October 2023, 15:53
Jeshi la polisi limejikuta likitumia nguvu kwa kutumia mabomu ya machozi kuwaondoa wananchi hali iliyoleta taharuki ya mapigano kati ya wananchi na jeshi la polisi.
Na Sifael Kyonjola
Mtaa wa Gombe kata ya Itezi jijini Mbeya umegeuka uwanja wa mapambano ya kivita baina ya wananchi zaidi ya mia moja hamsini wanaotakiwa kuondoshwa kwa amri ya mahakama baada ya wenzao watano kushindwa kesi.
Hili si maigizo bali ni hali halisi iliyotokea kata ya Itezi wananchi wakipambana na polisi kuzuia nyumba zao zisibomolewe na hapa wananchi hao wanapaza sauti zao kuwa mgogoro huo ulikuwa unahusisha watu watano na si wananchi wote.
Diwani wa kata ya ya Itezi Sambwee Shitambala ambaye ni mmoja wa Mawakili wa kujitegemea amesema wahanga wa mgogoro huo ni wananchi zaidi 150.
Aidha mkuu wa wilaya ya Mbeya Beno Malisa ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wilaya Mbeya amekiri kuwepo kwa vurugu eneo la Itezi na amewaomba wananchi kuwa watulivu kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kuona amri ya mahakama inatekelezwa.
Jiji la Mbeya limekuwa na migogoro mingi ya ardhi inayotokana na mipango mibovu ya mipango miji sanjari na maafisa ardhi kugawa viwanja mara mbili.