Bei za mafuta zasababisha mgomo wa daladala Mbeya, nauli zapandishwa kiholela
11 October 2023, 14:19
Wakazi wa Mbeya wamejikuta wakiamka na kukuta wanakosa usafiri wa kwenda kwenye shughuli zao hali iliyowasababishia kutumia usafiri wa bajaji kwa gharama kubwa.
Na Ezra Mwilwa
Wananchi jijini Mbeya wameiomba Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini LATRA kuchukua hatua za kisheria kwa madereva wa gari za abiria zinazofanya safari za Mbeya mjini hadi Mbalizi kutokana na kupandisha nauli kiholela.
Wakizungumza na kituo hiki wananchi hao wamedai kuwa hatua hiyo inawasababishia usumbufu wanapokuwa safarini kwani wanatozwa shilingi mia saba kati ya kituo na kituo badala ya shilingi mia tano.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wamesema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta ili kuwarahisishia gharama za uendeshaji.
Naye meneja wa LATRA Mbeya Omary Ayubu amesema mpaka sasa hakuna viwango vipya vya nauli walivyotangaza hivyo amewataka madereva kusubiri taarifa ya serikali kuhusu viwango vipya vya nauli badala ya kupandisha kiholela.