Bil. 6 kujenga miundombinu rafiki kwa makundi yenye ulemavu nchini
1 October 2023, 00:08
Kundi la walemavu wa kusikia ni kundi mojawapo ambalo limekuwa likikumbana na vikwazo vingi katika kupata huduma za kijamii kutokana na kukosa wataalam wengi wa lugha ya alama na hii imekuwa kikwazo na kuonekana watu wenye ulemavu hasa wa uziwi kutothaminiwa.
Na Hobokela Lwinga
Serikali imesema inathamini ustawi wa wananchi wote kwa kujenga mazingira bora na kuondoa changamoto zote zinazoyakabili makundi yote ya watu wenye ulemavu ikiwemo watu wenye ulemavu wa kutosikia. Kauli hiyo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Waziri Ndalichako amesema serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ambapo imetoa zaidi ya bilioni 6 ili kuboresha mazingira katika sekta mbalimbali ikiwemo kutoa ajira, fursa ya elimu pamoja na maeneo ya kutolea huduma za afya.
Akiwasilisha salamu za mkoa kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, mkuu wa wilaya ya Rungwe Jafar Haniu amesema serikali imefanikisha kundi la walemavu kupata mikopo kupitia halmashauri huku akiomba uwepo msisitizo kwenye taasisi kuwa na mtaalam wa lugha ya alama ili kurahisisha mawasiliano kwa kundi hilo.
Katika wasilisho la risala kwa mgeni rasmi kutoka kundi la viziwi imekiri kuwa vijana zaidi ya 294 makundi ya walemavu yamepewa ajira.
Aidha wamesema wanakabiliwa na changamoto ya jamii ya viziwi kukosa ushirikishwaji na kukosa huduma za afya kutokana na ukosefu wa wataalamu wa lugha ya alama.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani WHO wakili Mary Kessi ameishukru serikali kwa kuwa nchi ya kwanza kuwa na mpango kazi ambao unatoa huduma shirikishi kwenye kundi la walemavu.
Katika maadhimisho hayo taasisi ya kiraia ya Child Support kupitia kwa mkurugenzi wake Noela Msuya amesema taasisi yake imefanikiwa kuwafikia watoto zaidi ya elfu moja na kuwapatia elimu katika mfumo jumuishi.
Maadhimisho ya viziwi duniani ambayo kitaifa yamefanyika Mbeya yalitanguliwa na maandamano yaliyoanzia katika kituo cha daladala cha Kabwe na kisha kuhitimishwa katika viwanja vya Ruanda Nzovwe yakiwa yamebebwa na kauli mbiu isemayo ulimwengu ambao viziwi popote walipo wanaweza kutumia lugha ya alama.