Mch. Mwakipesile ahukumiwa miaka 3 jela
29 September 2023, 23:09
Kila nchi inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na sheria na katika sheria hakuna ambaye anakuwa juu ya sheria, hivyo kila mtu anapaswa kuheshimu taratibu na kuheshimu sheria.
Na Josea Sinkala
Mahakama ya Hakimu mkazi Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitatu Jela Mchungaji Mbarikiwa Mwakipesile (39) baada ya kukutwa na kosa la kuendesha huduma (Kikosi kazi cha Injili) bila usajili.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu mkazi Mkuu Paul Ntumo amesema Jamhuri ilikuwa ikimshtaki Mchungaji Mbarikiwa kwa kuendesha jumuia ya Kikosi kazi cha injili bila usajili maelezo ambayo hayakubishaniwa na uoande wa utetezi ambao ulidai unaendelea na taratibu za usajili huku wakiendelea kukutana kwa ajili ya huduma ya maombi.
Hakimu Ntumo amesema upande wa Mashtaka umethibitisha bila kuacha shaka mshtakiwa huyo kwamba alikuwa akiendesha shughuli za jumuiya ya kidini bila kuisajili ushahidi ambao ulielezwa na mashahidi mbalimbali wa Jamhuri kwa nyakati tofauti wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo.
Hata hivyo kwenye utetezi wake Mch. Mwakipesile aliiomba Mahakama Serikali kumuongezea muda kwani anaendelea kushughulikia taratibu za usajili wa Kikosi kazi cha Injili ambao wamekuwa wakikutana kama jumuia kwa ajili ya maombi pekee ushahidi ambao pia ulitolewa na mashahidi wake hasa waumini wa jumuiya ya Kikosi kazi cha Injili.
Mawakili Elisia Paul na Dominic Mushi ndio walikuwa waendesha mashtaka wa Serikali ambapo wakili Mushi ameiomba mahakama kutoa adhabu kama sheria inavyoelekeza ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine kwenye jamii kwa kukiuka sheria makusudi wakati akijua kuendesha huduma bila usajili ni kinyume cha sheria na Mchungaji Mbarikiwa alikuwa akiwakilishwa na wakili Boniface Mwabukusi ambaye hata hivyo hakuwepo Mahakamani kwenye usomwaji shauri hilo.
Baada ya kutiwa hatiani Mch. Mbarikiwa aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na alikuwa akiendelea na taratibu za usajili wa huduma ya kikosi kazi kuwa kanisa kamili na ni mtumishi anayetegemewa na watu mbalimbali ikiwemo familia yake.
Kosa alilokuwa akituhumiwa Mchungaji huyo na sasa limeelezwa kuthibitishwa ni kinyume na kifungu namba 25 (1) cha sheria ya usajili wa Taasisi za kijamii sura namba 337 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Baada ya kuridhika na ushahidi wa Jamhuri na utetezi pia maombolezo ya Mtumishi huyo, Hakimu Paul Ntumo amemhukumu Mch.Mbarikiwa Dickson Mwakipesile (39) mkazi wa Isyesye jijini Mbeya kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitatu na siku 14 jela na kuweka wazi haki ya kukata Rufaa kwa upande usioridhika na hukumu hiyo.