Biblia ya Agano Jipya yazinduliwa kwa lugha ya Kisafwa Mbeya
26 September 2023, 10:24
Tanzania ina makabila zaidi ya 120 na kila kabila lina mila na destri zake, katika kudumisha utamaduni, Umoja wa kabila la Wasafwa Mbeya umeandika Biblia ya Agano la Jipya kwa lugha ya Kisafwa.
Na Josea Sinkala
Umoja wa Maendeleo ya Kabila la Wasafwa mkoa wa Mbeya umezindua Biblia ya Agano Jipya iliyotafsiriwa kutoka kwenye lugha ya kiswahili baada ya kuiandaa tangu mwaka 2003.
Uzinduzi huo umefanyika katika kanisa la Moravian Ushirika wa Iwala Mbeya vijijini ukiongozwa na mgeni rasmi Mhe. Mwalingo Kisemba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya ambaye amewapongeza waandaaji wa biblia hiyo ambayo itatunza utamaduni wa kabila hilo na taifa kwa ujumla.
Akihubiri kwenye sherehe hiyo, Mch. Daudi Kapusi wa kanisa la Pentecost Holiness Mission Iwindi amesema hata mahubiri yanapohubiriwa kwa lugha ya asili kwa watu wenye kabila hilo yanaeleweka zaidi na yatadumisha tamaduni bila kumkosea Mungu wala kuendekeza ubaguzi wowote katika jamii.
Katibu wa Umoja wa Maendeleo kwa Wasafwa mkoa wa Mbeya Mch. Raiton Yongo amesema katika maandalizi ya biblia hiyo wamepitia katika changamoto mbalimbali hadi kukamilika kwake kwa muda wa miaka 24.
Watumishi mbalimbali wakiwemo viongozi wamewapongeza kwa juhudi hizo na kuomba wakristo kununua Biblia hizo za Agano Jipya bila kujali utofauti wa kikabila.