Jimbo la Mbarali lapata mrithi wa aliyekuwa Mbunge Francis Mtega
20 September 2023, 18:11
Tume ya Taifa ya uchaguzi ilitangaza uchaguzi mdogo baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega kufariki kwa ajali akielekea shambani kwake.
Na Daniel Simelta
Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Missana Kwangura amemtangaza Bahati Ndingo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mshindi kufuatia uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika Septemba, 19,2023.
Bahati Ndingo ametangazwa mshindi baada ya kupata kura 44, 334 huku mshindani wake wa karibu Modestus Kilufi kutoka chama cha ACT – Wazalendo akipata kura 10, 014.
Baada ya ushindi huo Bahati Ndingo amewashukuru wananchi wa Jimbo la Mbarali kwa kumwamini na kumpa ridhaa ya kuwawakilisha kutika mhimili wa bunge.
Kwa upande wake katibu wa chama cha Demokrasia makini Amely Hassan ameishukuru tume ya uchaguzi kwa kusimamia uchaguzi huo mpaka hatua ya kutangazwa matokeo hayo.
Aidha Modestus Kilufi mgombea kutoka chama cha ACT – Wazalendo aliyeshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi huo amesema uchaguzi huo ulikuwa na dosari ikiwemo muda wa uapisho wa mawakala.
Pia Kilufi amesema amesikitishwa na kushangaa kuwa baadhi ya maeneo ya vituo vya kupigia kura idadi ya kura kuwa nyingi tofauti na wapiga kura waliopo.