Baraka FM

Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yaongoza maambukizi ya Ukimwi

2 December 2024, 14:53

Jamii inapaswa kuwa chachu ya mabadiliko ya mapambano ya Ukimwi kwa kutoa elimu kwa kizazi cha sasa na cha badae.

Na Ezekiel Kamanga

Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya (MZRH) imefanya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa kutoa elimu ya ufuasi mzuri wa dawa za kinga ya mwili, mgeni rasmi akiwa ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya Dkt Uwesu Mchepange.

Maadhimisho hayo yamefanyika Kitengo cha Watoto Huduma za nje za kibingwa ambapo hutoa huduma zote zikiwemo dawa za kufubaza vizusi vya Ukimwi sanjari na elimu ya Mapambano dhidi ya Ukimwi pamoja na ushauri nasaha.

Dkt Uwesu Mchepange amesema mapambano dhidi ya Ukimwi yameanza miaka arobaini na moja iliyopita na kauli mbiu ya mwaka huu”Chagua njia sahihi kutokomeza Ukimwi”.

Mchepange amesema bado mikoa ya nyanda za juu ipo juu katika maambukizi ya Ukimwi ukitangulia Mkoa wa Njombe,Iringa na Mbeya hivyo kila mtu anapaswa kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya Ukimwi.

Aidha amewataka wananchi wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi kuwa wafuasi wazuri wa dawa ili watoto wakue vizuri na kuishi kwa muda mrefu.

Pia Dkt Uwesu Mchepange amehitimisha maadhimisho hayo kwa kuwasha mshumaa wa upendo ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka waliotangulia mbele za haki.

Kwa upande wake Mratibu wa maadhimisho hayo Dkt Nazareth Mbilinyi amesema lengo la kufanya maadhimisho hayo ya siku ya Ukimwi ni kuwakutanisha vijana walio kwenye klabu za watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi ili kuwapa elimu na ushauri nasaha pia kupunguza kasi ya maambukizi na wawe wafuasi wazuri wa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.

Naye Huruma Nyondo mshauri nasahasa ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwahimiza na kuwasisitiza watoto na vijana kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na kunywa dawa kwa wakati.

Aidha amesema wanafanya ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto pindi wanapozaliwa katika kila hatua ili wasikatize dawa na kufanya ukuaji wa watoto unakuwa mzuri zaidi.

Hafla hiyo imejumuisha wafanyakazi wa MZRH ambao waliwatunuku zawadi mbalimbali watoto wenye ufuasi mzuri wa dawa za kufubaza Ukimwi awali watoto wamejumuika katika michezo mbalimbali kama kuimba na maigizo.

Kwa Mkoa wa Mbeya maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani kimkoa yamefanyika Kata ya Ifumbo Wilaya ya Chunya na Kitaifa yamefanyika Songea Mkoani Ruvuma.