EAGT hema ya furaha yafanya maombi kuelekea mwisho wa mwaka
4 November 2024, 20:13
Tunapoomba kwa bidii, Mungu anatenda zaidi ya tunavyoweza kutarajia.
Na Yuda Joseph Mwakalinga
Waumini Kanisa la EAGT Hema ya Furaha, lililopo Airport ya Kwanza wamefanya ibada maalumu ya maombi ya kuepusha mishale ya adui, maalumu kwa kipindi cha mwisho wa mwaka.
Ibada hiyo imeongozwa na Mwimbaji na Mchungaji Happy Kamili ambaye alihubiri kuhusu ulinzi wa Mungu dhidi ya mishale ya kiroho na kimwili inayoweza kushambulia wakati wa kipindi hiki cha mabadiliko ya mwaka.
Katika mahubiri yake Mchungaji Happy Kamili amesisitiza umuhimu wa waumini kuomba kwa ajili ya mauti kwenye familia, uchumi, afya, na elimu.
Amesema kuwa maombi haya yanawasaidia waumini kutafuta ulinzi wa Mungu dhidi ya vifo visivyotarajiwa kwenye familia zao, na pia kuomba baraka za kiuchumi, afya bora, na elimu yenye mafanikio kwa watoto wao.
Aidha Mchungaji ametilia mkazo maombi kwa ajili ya taifa, akihimiza waumini kulia kwa Mungu kwa ajili ya amani, haki, na mwongozo wa kiroho tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani.
Alisema, “Tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao, ni jukumu letu kama watu wa Mungu kumwomba kwa ajili ya uongozi bora na kwa amani itawale nchini.”
Ibada hiyo ilihudhuriwa na kwaya, waimbaji binafsi, na bendi, ambao waliwabariki waumini kwa nyimbo za sifa na ibada.
Nyimbo hizo zimeimarisha roho za waumini, wakiungana kwa pamoja kumwomba Mungu kwa ajili ya ulinzi na baraka za kipekee wakati huu wa mwisho wa mwaka.
Mchungaji amehitimisha kwa maombi ya pamoja, akiwataka waumini waendelee kutegemea maombi ili kuepusha mishale ya adui katika maisha yao ya kila siku, na kumtumainia Mungu kwa mwaka mpya.