Zaidi ya wanafunzi wa kike 130 wapatiwa taulo za kike Yalawe sekondari Mbeya Dc
26 October 2023, 13:40
Mtoto wa kike amekuwa akipitia madhira kadhaa ambazo zimekuwa zikimfanya kukosa masomo,wengine kutokana na ugumu wa maisha waliyonayo wazazi wao wamekuwa wakiacha shule na kujikuta wakishindwa kutimiza ndoto zao,hali hiyo imekuwa ikichochea uwepo wa ndoa za utotoni.
Na Hobokela Lwinga
Zaidi ya wanafunzi wa kike 130 katika shule ya sekondari yalawe inayopatikana kata ya santilya halmashauri ya mbeya wamepatiwa msaada wa taulo za kike uliotolewa na kituo cha radio Baraka.
Akizungumza na kwa niaba ya kituo cha radio Baraka wakati wa kukabidhi msaada huo ulioratibiwa na kipindi cha radio cha kivulini,meneja wa vipindi Mpoki Japhet amesema kituo hicho kimekuwa na utaratibu wa kurudisha shukrani kwa jamii kwa kutoa msaada kwenye makundi mbalimbali yenye uhitaji.
Kwa upande wake mwalimu Betina Kyando katika shule hiyo amesema msaada huo utapunguza changamoto ya wanafunzi wengi wa kike ambao walikuwa wanakosa masomo kwa takribani siku kuanzia tano kipindi cha hedhi zao.
Aidha baadhi ya wanafunzi ambao wamenufaika na msaada huo wameishukru Baraka fm kwa kuwakumbuka na kuwaona licha ya kuwa wapo kijijini huku wakiomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidia kutatua changamoto anazokumbana nazo motto wa kike.
Msaada huo umetolewa na kituo hicho kutokana na changamoto ambayo mtoto wa kike amekuwa akikumbana nayo hasa akiwa kwenye siku zake.