Baraka FM

Wananchi Chunya wazikimbia nyumba zao kisa mwekezaji

14 December 2024, 10:33

Mgogoro mkubwa kati ya wananchi na mwekezaji umezuka, huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Na Ezekiel Kamanga

Wananchi wa Kijiji cha Ifumbo Kata ya Ifumbo Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wamelazimika kuzikimbia nyumba zao baada ya Jeshi la Polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi kando ya mto Zira wakidai mwekezaji mwenye asili ya China aondoke eneo hilo kwa madai ya kuharibu mazingira.

Awali wananchi hao wakiwa ofisi za kijiji cha Ifumbo mbele ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chunya na Diwani wa Kata ya Ifumbo Winston Mpyira wamedai eneo analochimba madini mwekezaji ndilo eneo walikatazwa kuchimba na wao sasa wanashangazwa na kitendo cha mwekezaji kuanza kuchimba ilhali Serikali ya Kijiji haina taarifa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ifumbo Bahati Sinkwembe amesema hajapata waraka wowote juu ya uchimbaji wa mwekezaji huyo hali iliyowafanya wananchi watahatuki na kuandamana hadi ofisi ya kijiji.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ifumbo Winston Mpyira na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chunya baada ya kusikiliza wananchi wamesema madai yao yana msingi na wao hawawezi kutoa majibu hivyo wakaomba wananchi kuwa watulivu wakati wanafanya mawasiliano na watu wa mazingira, madini na Mkuu wa Wilaya ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Baada ya mkutano huo kwa pamoja walilazimika kumsimamisha mwekezaji asiendelee na uchimbaji hadi pale utakapopatikana muafaka wa suala hilo na stahiki za kijiji cha Ifumbo.

Wakati hayo yakijiri eneo la mgogoro wananchi walifunga njia zote zinazoingia na kutoka Ifumbo kwa kutumia miti na magogo hali iliyowafanya maaskari polisi kuwatawanya kwa mabomu wananchi hao na wananchi kuchoma moto ghala la kuhifadhia vifaa la mwekezaji lililokuwa na vifaa vya ujenzi kama mabati na mbao.

Zaidi ya pikipiki hamsini zilizokuwa eneo la mgogoro zilizuiliwa na Jeshi la Polisi na kuwakamata baadhi ya wamiliki wa pikipiki hizo.

Juhudi za kumtafuta Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Mubarak Alhaj Batenga zinaendelea ili kujua hatma ya mgogoro huo.

Kijiji cha Ifumbo ni moja ya vijiji vingi vya wilaya ya Chunya vyenye migogoro ya ardhi hususani maeneo ya machimbo ya dhahabu.