Baraka FM

Ken Gold yapania kuifunga Yanga uwanja wa Sokoine Mbeya

24 September 2024, 15:16

Ligi kuu Tanzania bara yaani NBC premier league inatarajiwa kuendelea kesho katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya kwa wenyeji Ken Gold kuwa kuwakaribisha Yanga kutoka Dar es salaam.

Na Ezekiel Kamanga

Mchezo Ligi ya NBC utaozikutanisha timu ya Ken Gold na Yanga jumatano hii unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutoka pande zote mbili ambapo wenyeji hawatakuwa tayari kupoteza mchezo wa tano mfululizo ilhali timu ya Yanga ikitaka kutetea ubingwa wake kwa kujiongezea alama tatu muhimu.

Kutokana na shauku hiyo Mkurugenzi wa timu ya Ken Gold Keneth Mwakyusa amelazimika kufika uwanja wa Sokoine katika mazoezi kwa lengo la kuwatia moyo wachezaji, viongozi na dawati la ufundi.

Mwakyusa amesema Ligi ni ngumu lakini chochote kinaweza tokea katika mchezo wa soka ingawa wamepoteza michezo yote lakini haiwazuii wao kushinda mchezo uliopo mbele yao na kwamba makosa ya usajili ndiyo sababu ya kutopata matokeo.

Mwalimu Jumanne Chale amesema wachezaji wana ari ya mchezo na anaendelea kufanya marekebisho ya kupitia michezo iliyopita katika maeneo ya ulinzi kiungo na ushambuliaji.

Aidha amesema anajaribu kuwapa maelekezo kwa kuwa ameipokea timu kutoka kwa Mwalimu mwingine.

Naye Charles Masai kwa niaba ya wachezaji wenzake amesema wapo tayari kukabiliana na mchezo huo na wanaendelea kufanya kazi maelekezo ya Mwalimu.

Timu ya Yanga tayari imewasili Jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika uwanja wa Sokoine.

Meneja wa uwanja wa Sokoine Modestus Mwaluka amesema maandalizi ya uwanja yamekamilika ikiwa ni pamoja na ukataji nyasi.

Mwaluka amesema marekebisho yanayofanyika ni sehemu ya majukumu yake ya kila siku kwani amewahi kuwa Meneja bora wa Uwanja mara tano.

Kiingilio kinatajwa kuwa shilingi elfu thelathini VIP na shilingi elfu kumi mzunguko.