Baraka FM

Sangoma adaiwa kumbaka binti yake Mbeya

13 July 2024, 05:18

Jengo la mahakama ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya(picha na Ezekiel Kamanga)

Katika hali ya kushangaza binti mmoja mkoani Mbeya anadaiwa kufanyiwa kitendo cha ukatili na mzazi wake wa kumzaa (Baba) kwa kudaiwa kufanya naye tendo la ndoa.

Na Ezekiel Kamanga

Masumbuko Sompo (51) mganga wa jadi mkazi wa kijiji cha Nyombwe kata ya Sangambi wilaya ya Chunya mkoani Mbeya anatuhumiwa kumbaka binti yake wa kumzaa mwanafunzi kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17.

Binti amedai kufanyiwa tukio hilo na baba yake Juni 23, 2024 usiku wa manane baada ya kumtoa kwa nguvu chumba chake cha nje ambacho hakina mlango.

Binti huyo anaishi na mama wa kambo baada ya mama yake mzazi kufariki akiwa na umri wa miaka minane. Amedai kuwa siku anafanyiwa ukatili huo alikuwa hajitambui na nguo za baba yake na za kwake zilichukuliwa na wake zake ambazo walimpatia asubuhi.

Binti anayedaiwa kufanyiwa kitendo cha ukatili na mzazi wake (Picha na Ezekiel Kamanga)

Baada ya siku mbili taarifa ilitolewa polisi Chunya na ofisi za Ustawi wa Jamii ambapo alipimwa kisha kufunguliwa jalada la uchunguzi. Baada ya uchunguzi mtuhumiwa amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Chunya.

Mahakama ya wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya(picha na Ezekiel Kamanga)

Bibi ambaye ni shangazi wa marehemu Selina Mvwango amesikitishwa na tukio hilo na kuomba sheria ichukue mkondo wake.

Selina amedai ndugu wa mganga wamekuwa wakijaribu kulificha jambo hilo ili kumnusuru ndugu yao.

Hata hivyo kaka wa mwanafunzi aliyebakwa alimpiga mwanafunzi huyo kwa kile alichodai anataka kumfunga baba yake.

Kwa upande wake Said Mohammed Madudu Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya haki za binadamu amesema jamii isifumbie macho vitendo hivyo kwani vinazidi kushamiri siku hadi siku.

Amesema baadhi ya vitendo hufanywa na ndugu wa karibu na wengine wakiwa ni watumishi wa umma hivyo ni vema jamii ikakemea kwa nguvu zote.