Waandishi wa habari Mbeya kuwezeshwa kuandika habari za uchaguzi
15 May 2024, 19:06
Tanzania inatarajia kuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 na moja ya tasnia inayotazamwa kutoa elimu ni vyombo vya habari kutokana na kuwa karibu na jamii.
Na Hobokela Lwinga
Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mbeya imesema iko tayari kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari ili kuandika habari zenye mlengo wa kutoa elimu juu ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 wa madiwani,wabunge na Rais.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe.Beno Malisa wakati akimuwakilisha Mkuu mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera kwenye sherehe za Uhuru wa vyombo vya habari mkoa Mbeya zilizofanyika katika ukumbi wa coffee gadern jijini Mbeya.
Aidha mhe.Malisa amewataka waandishi hao wa habari mkoani hapa kutumia fursa zinazojitokeza kwenye maeneo yao.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya amewataka waandishi kuwa weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya ACP Benjamin Kuzaga Amesema wanahabari wamekuwa watu muhimu kwenye jamii kutokana na mchango mkubwa wa kuhabarisha umma huku akiwataka kuendelea kufichua vitendo vya uharifu vinavyofanywa na watu wasio wema.
Awali akiwasilisha risala ya waandishi wa habari kwa mgeni rasmi,Katibu mkuu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Elizabeth Nyivambe amesema uwepo wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya umesababisha taaluma ya habari kukua sambamba na kuongezeka kwa ufikishwaji wa taarifa kwa jamii.
Katika maadhimisho hayo yamekwenda na kauli mbiu inayosema Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.