Dkt.Tulia atoa ajira kwa vijana 20 wanagenzi chuo cha ufundi Magereza
3 May 2024, 09:37
Kama ambavyo imekuwa desturi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki na kuwezesha jamii katika utatuzi wa changamoto hali hiyo ameendelea kuonesha kwa kujali makundi yote yakiwemo ya vijana.
Na Ezekiel Kamanga
Rais wa Mabunge Duniani Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tulia Trust na Mbunge wa Mbeya Mjini amewawezesha vijana ishirini Jiji la Mbeya kupata ajira baada ya kuhitimu mafunzo mbalimbali ya Uanagenzi katika Chuo cha Ufundi Ruanda kinachomilikwa na Jeshi la Magereza.
Mbali ya kuwapatia ajira vijana ishirini pia amewawezesha fedha za nauli kwa kuwakatia tiketi pamoja na fedha za kujikimu wakiwa safarini Mkoa wa Pwani ambako wanakwenda kufanya kazi kiwandani.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson Katibu wa Mbunge Stephen Chambanenge amesema hii ni awamu ya pili kwa Dkt Tulia kutoa fursa ya ajira kwa vijana awali vijana arobaini walinufaika na fursa hiyo.
Chambanenge amesema huu ni utekelezaji wa Mbunge kipindi cha kampeni kuwawezesha wananchi kiuchumi na ajira kwa vijana wa Jiji la Mbeya kwa kuwa yeye ni Mbunge wa kujiongeza.
Asumini Mbunda ni mkufunzi Mkuu Chuo cha Ufundi Magereza Ruanda akiwaaga vijana hao amewaasa kuwa mabalozi wazuri wa Chuo pamoja na Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson.
Naye Robert Temba mratibu wa mafunzo amemshukuru Dkt Tulia Ackson kwa kuwapatia fursa ya pili ya vijana waliohitimu mafunzo ya Uanagenzi katika mpango maalumu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.
Rehema Kingu Mrakibu Msaidizi wa Chuo cha Ufundi Magereza Ruanda Mbeya amesema Chuo kinatoa fani saba ambazo ni Uchomeleaji,Umeme wa Majumbani,Ushonaji,Rangi,Bomba,Uashi na Useremala ambapo hutoa mafunzo kwa raia na wafungwa.
Amewaasa vijana kushirikiana watakapokuwa huko huku akiwasisitiza wazazi kuwasomesha watoto ili waweze kujiajiri akisisitiza kauli mbiu ya Chuo kuwa “Ufundi ni Ajira”.
Nao vijana walionufaika na fursa hiyo akiwemo Joel Mbughi ambaye ni mhitimu wa Uashi amesema yale walifundishwa watayafanyia kazi.
Neema Joseph ambaye amehitimu fani ya Ufundi Bomba amelishukuru Jiji la Mbeya kwa kuwapa fursa ya mafunzo na Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt Tulia Ackson kwa kuwapatia fursa ya ajira sanjari na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupambana na tatizo la ajira kwa vijana.