Wawili wakamatwa utoroshaji madini Mbeya
13 November 2023, 17:46
Na mwandishi wetu
Watu wawili wa familia moja wamekamatwa na kikosi kazi cha madini kwa kushirikiana na maafisa madini mkoa wa kimadini wa Mbeya wakitorosha vipande 28 vya dhahabu iliyochomwa yenye uzito kilogramu 1.08373 yenye thamani ya shilingi mil. 142.229.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Juma Homera akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake amesema, watuhumiwa hao mtu na mdogo wake (majina yanahifadhiwa) walikamatwa jana Novemba 11, 2023 majira ya saa 6:00 usiku na kikosi kazi cha madini.
Homera amesema vipande hivyo vya dhahabu 28 vina uzito wa kilogramu 1.08373 thamani yake ni shilingi mil.142.229 za kitanzania mrabaa ukiwa ni shilingi milioni nane, ada ya ukaguzi milioni 2,844,5866.36 kodi ya huduma shilingi 426,687.96 na kodi ya zuio shilingi milioni 13.231.
Pia Homera amesema kuwa wizi huo unasababisha upotevu wa takwimu halisi za uzalishaji wa madini ya dhahabu na kupunguza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa. Ameongeza kuwa watuhumiwa wote wawili wanashilikiwa kituo cha polisi Mbeya na wamefunguliwa jadala MBE/IR/5162/2023 kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Benjamin Kuzaga amesema wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kutorosha madini ni Edward Kessy na Feisal Abdullah wakazi wa Makongolosi wakiwa na dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 141.