Wanafunzi shule za msingi wilaya ya Songwe kunufaika na vyandarua 32,670
5 November 2023, 13:44
Wilaya ya Songwe imezindua kampeni ya usambazaji na ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule zote za msingi za Serikali na binafsi lengo likiwa ni kutokomeza maambukizi ya malaria katika wilaya hiyo.
Na Mwandishi wetu,Songwe
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, CPA. Cecilia Kavishe amesema kuwa Wilaya hiyo imefanikiwa kupunguza maambukizi ya malaria hasa kwa watoto huku akiwasisitiza wananchi kutumia vyandarua ili kutokomeza ugonjwa huo.
CPA. Kavishe amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya usambazaji wa vyandarua 32, 670 kwa wanafunzi wote wa shule za msingi katika wilaya hiyo vilivyotolewa na Bohari ya Dawa (MSD) ili kusaidia kutokomeza maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa mwaka 2019 maambukizi ya malaria yalikuwa jumla 25,000 huku watoto wakiwa 2,089 lakini mwaka 2022 yamepungua mpaka kufikia jumla 9,509 ambapo maambukizi hayo kwa watoto ni 848.
Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Miradi wa Bohari ya Dawa (MSD), Dkt. Pamella Sawa amesema kuwa Serikali inataka kila mtoto awe analala kwenye chandarua ndio maana imeanza kugawa vyandarua kwa wanafunzi ili kutokomeza malaria.
Mfamasia wa MSD Kanda ya Mbeya, Caroline Corlnelius Amesema Bohari ya Dawa (MSD) imetoa jumla ya vyandarua 32,670 ambavyo vitasambazwa na kupewa wanafunzi wa shule za msingi katika Wilaya ya Songwe ili kusaidia kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa malaria.