Sekondari ya Shisyete yakabiliwa na uhaba wa walimu, vifaa
24 October 2023, 16:47
Wakati mapambano ya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri hali hiyo si nzuri katika shule ya sekondari Shisyete iliyoko Mbeya Dc nakilio hicho kikitolewa na wanafunzi wa shule.
Na josea sinkala
Shule ya sekondari Shisyete kata ya Shizuvi wilayani Mbeya inakabiliwa na upungufu wa walimu, maabara na vifaa vingine kadhaa vya kujifunzia katika kuboresha elimu shuleni hapo.
Hayo yameelezwa na wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Shisyete wakati wakitoa taarifa yao kwenye mahafali yao kupitia risala yao kwa mgeni rasmi Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza ambapo wamesema shule yao haina maabara na walimu hasa wakike.
Mkuu wa Shule ya Shisyete sekondari Mwal.Onesmo Mwano ameishukuru Serikali kwa kufikisha huduma ya maji shuleni kwake na kuiomba kuendelea kutatua kero zilizosalia shuleni hapo ili kuboresha mazingira ya utoleaji elimu.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Oran Njeza, Diwani wa Kata ya Shizuvi Noah Mwashibanda amesema ni dhamira ya Serikali kuendelea kutatua changamoto zilizopo ikiwemo umeme.
Kuhusu umeme amesema wataalam wako katani humo kusambaza nguzo huku Mbunge Njeza akichangia sh.million moja kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa shule kuanza kujenga jengo moja la bweni shuleni hapo.
Furaha Kameka kutoka Ofisi ya Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amesema kero ambazo bado zipo zitaendelea kushughulikiwa kwa awamu ikiwemo ubovu wa barabara.
Wazazi na walezi wanasema wataendelea kushirikiana kuhakikisha wanajenga mabweni ili kuwasaidia watoto wao kupata elimu katika mazingira bora na kuiomba Serikali kuwaunga mkono.