Zenj FM

Dokta Lulu:kuwahi hospitali ni muhimu katika mapambano dhidi ya saratani kwa watoto

30 September 2026, 20:53

Daktari Bingwa wa Saratani na Magonjwa ya Damu kwa Watoto, Dkt. Lulu Chirande,akizungumza katika mafunzo kwa wahudumu wa afya, viongozi wa dini  na waandishi wa habari katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja,

Daktari Bingwa wa Saratani na Magonjwa ya Damu kwa Watoto, Dkt. Lulu Chirande, amewaasa wazazi na walezi kutopuuza dalili za saratani kwa watoto na kuwahi kuwapeleka hospitali kwa uchunguzi. Amesema utambuzi wa mapema huongeza nafasi ya mtoto kupona na kurejea katika maisha ya kawaida.

Na Mary Julius.

Daktari Bingwa wa Saratani na Magonjwa ya Damu kwa Watoto, Dkt. Lulu Chirande, amewaasa wazazi na walezi kuwahi kuwapeleka watoto hospitali wanapoona dalili za saratani.

Akizungumza katika mafunzo kwa wahudumu wa afya, viongozi wa dini  na waandishi wa habari katika ukumbi wa Skuli ya Tumekuja, Dkt. Lulu amesema utambuzi wa mapema huongeza nafasi ya mtoto kupona na kurejea katika maisha ya kawaida.

Amesema dalili zinazopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na mabadiliko yasiyo ya kawaida machoni, uvimbe tumboni, homa za mara kwa mara, kuvimba tezi, kutokwa damu, maumivu ya mifupa yanayoendelea, degedege, maumivu ya kichwa na kutapika mara kwa mara.

Dkt. Lulu amesema takribani watoto 400,000 duniani hupata saratani kila mwaka, huku Tanzania takribani watoto 1,000 wakigundulika kwa mwaka, akisisitiza kuwa baadhi ya watoto hawafiki hospitalini kwa wakati.

Sauti ya Daktari Bingwa wa Saratani na Magonjwa ya Damu kwa Watoto, Dkt. Lulu Chirande,

Kwa upande wake, Dkt. Mohamed Said Suleiman, Daktari bingwa wa magonjwa ya damu Hospitali ya Wilaya Ijitimai, amesema Zanzibar watoto 115 wamewahi kupata saratani na kupona, huku vifo 110 vikirekodiwa kati ya mwaka 2018 na 2026.

Sauti ya Dkt. Mohamed Said Suleiman, Daktari bingwa wa magonjwa ya damu Hospitali ya Wilaya Ijitimai,

Naye Dkt. Regina Elia, Daktari bingwa wa magonjwa ya damu na saratani, amesema saratani zinazowapata watoto ni pamoja na ya macho, figo, damu, mifupa, ubongo na tezi, akiwataka wazazi kutopuuza mabadiliko yoyote yasiyo ya kawaida kwa mtoto.

Sauti ya Dkt. Regina Elia, Daktari bingwa wa magonjwa ya damu na saratani, a

Nao Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kutumia elimu waliyoipata kuwaelimisha wananchi na kuhamasisha wazazi kuwapeleka watoto hospitali mapema.

Sauti ya Washiriki.