Zenj FM
Zenj FM
23 November 2026, 16:15

Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), kuanzia Desemba Mosi, utawajumuisha wenza wa ndoa wa wanachama wake katika huduma za matibabu bila michango ya ziada, hatua inayolenga kuimarisha afya na ustawi wa familia. Mpango huo unatarajiwa kuongeza zaidi ya wanufaika wapya 100,000 na kuhakikisha wanachama, wenza wao pamoja na watoto wanapata huduma za afya kupitia mchango mmoja.
Na Mary Julius.
Mkurugenzi Mkuu wa,Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), Dk. Heri Marwa amesema kuanzia Desemba Mosi mwaka huu, mfuko huo utawajumuisha wenza wa ndoa wa wanachama wake katika huduma za matibabu bila malipo ya ziada.
Akizungumza na waandishi wa habari Michenzani,dk Heri amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha huduma za afya kwa familia, ambapo mwanachama, mwenza wake na watoto watanufaika kupitia mchango mmoja bila ukomo wa idadi ya watoto.
Amesema kwa sasa mfuko una wanachama wachangiaji 107,076 na unatarajia kuongeza zaidi ya wanufaika wapya 100,000 kupitia mpango huo.
Aidha, amesema serikali hutenga shilingi bilioni 5.3 kila mwezi kugharamia matibabu ya wananchi ambao hawana bima ya afya, hivyo mpango huo utasaidia kupunguza mzigo huo na kuelekeza fedha kwa wenye uhitaji zaidi.
Dk. Marwa amewataka wanachama ambao hawakuwasilisha taarifa za wenza wao wakati wa usajili kuwasiliana na mfuko kwa maelekezo ya kuwasilisha cheti cha ndoa, huku walioorodhesha wenza wao wakitakiwa kuthibitisha taarifa zao kwa njia ya simu.
Amesema ZHSF pia inaendelea kushirikiana na ZSSF, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, BPRA na ZCSRA kuimarisha mifumo ya usajili na ukusanyaji wa michango, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia afya bora kwa wote ifikapo mwaka 2030.