Zenj FM

Mapinduzi ya huduma za uzazi Zanzibar ZHSF Mother sasa wilaya zote 11

9 October 2026, 16:21

Picha na Mary Julius

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanua mpango wa ZHSF Mother kutoka wilaya mbili hadi wilaya zote 11 za Zanzibar, hatua inayolenga kuwaondolea wanawake wajawazito, hususan kutoka kaya zenye kipato cha chini, kikwazo cha gharama za matibabu na kuwawezesha kupata huduma bora za afya kuanzia ujauzito hadi siku 42 baada ya kujifungua. Mpango huo, ambao tayari umewafikia zaidi ya wanawake wajawazito 5,000 wenye uhitaji, ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Na Mary Julius.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepanua mpango wa ZHSF Mother kutoka wilaya mbili za awali hadi wilaya zote 11 za Zanzibar, hatua inayolenga kuhakikisha wanawake wajawazito, hususan wenye uwezo mdogo wa kifedha, wanapata huduma za afya kwa wakati bila kikwazo cha gharama.

Akizungumza katika uzinduzi wa upanuzi wa mpango huo uliofanyika Hospitali ya Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za afya kwa mama na mtoto.

Waziri Mazrui amewataka watendaji wa Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku akisisitiza umuhimu wa Community Health Workers kuwafuatilia wanawake wajawazito tangu wanapogundua ujauzito hadi wanapojifungua.

Amesema hakuna mwanamke anayepaswa kuchelewa kliniki au kujifungua nyumbani kwa sababu ya kukosa uwezo wa kifedha, akivitaka vituo vya afya kuwapokea na kuwahudumia wanawake kwa wakati.

Sauti ya Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui,

Naye Kaimu Mkurugenzi wa PharmAccess Tanzania, Sella Bagiri, amesema PharmAccess itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na ZHSF katika kuhakikisha mpango huo unafikia wanawake wengi zaidi na kuchangia juhudi za kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa PharmAccess Tanzania, Sella Bagiri.

Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF, Heri Marwa, amesema ZHSF imejipanga kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi, ikiwemo kuboresha vifaa na huduma katika vituo vya afya.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF, Heri Marwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa PharmAccess Zanzibar Jonia Bwakea amesema awamu ya kwanza ya mpango huo imeonyesha mafanikio kwa kuwafikia wanawake wenye uwezo mdogo wa kifedha na kuwawezesha kupata kifurushi cha huduma za afya kuanzia ujauzito hadi siku 42 baada ya kujifungua.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa PharmAccess Zanzibar Jonia Bwakea

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Afya, Mayasa Suleiman, amesema ZHSF Mother ni sehemu ya mikakati ya Zanzibar kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Amesema mradi umebaini kuwa baadhi ya wanawake huchelewa kufika vituoni kwa ajili ya huduma za uzazi, hivyo amewataka wanawake kuanza kliniki mapema na kuhakikisha wanakuwa na kadi za matibabu kwa ajili ya ufuatiliaji wa huduma wanazopata.

Sauti ya Mayasa Suleiman,

Naye mnufaika wa mpango huo, Mture Haji, amesema ZHSF Mother imemsaidia kupata huduma tangu akiwa na ujauzito wa miezi minne hadi kujifungua salama.

Amesema yeye na mume wake pia walipata elimu kuhusu afya ya mama na mtoto, huku akiwahimiza wanawake wajawazito kutobaki majumbani, bali kuanza kliniki mapema ili kupata huduma na ushauri wa wataalamu.

Sauti ya Mnufaika.

Mpango huo ulianza mwaka 2025 katika Wilaya ya Kaskazini B Unguja na Micheweni Pemba, na sasa unapanuliwa katika wilaya tisa zilizobaki za Unguja na Pemba, huku utekelezaji wake ukitarajiwa kuendelea hadi Agosti 2027.