Zenj FM
Zenj FM
2 June 2026, 19:20

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme ya kuaminika na nafuu. Hatua hiyo imejidhihirisha kupitia ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na Airtel Money unaowezesha ununuzi wa umeme wa TUKUZA kwa njia za kidijitali.
Na Mary Julius.
Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Seif Kombo Pandu amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha sekta ya nishati kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za umeme za kuaminika, nafuu na endelevu kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikiano na sekta binafsi.
Akizungumza kwa Niaba wa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Seif Kombo Pandu ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na Airtel Money unaowezesha wananchi kununua umeme wa TUKUZA kwa njia za kidijitali.
Amesema Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 inalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za nishati huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wawekezaji mbalimbali kufanikisha malengo hayo.
Naibu Waziri Seif amesema ushirikiano kati ya ZECO na Airtel Money ni hatua muhimu ya kujenga Zanzibar ya kisasa inayotumia teknolojia kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, ameipongeza Airtel Tanzania kwa ubunifu huo pamoja na taasisi za kifedha ikiwemo People’s Bank of Zanzibar (PBZ) kwa mchango wake katika kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuwawezesha wananchi kutumia huduma rasmi za kifedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba, amesema kampuni hiyo imejipanga kusogeza huduma muhimu karibu zaidi na wananchi wa Unguja na Pemba ili kurahisisha maisha yao kupitia huduma za kidijitali.
Amesema uwezeshaji wa ununuzi wa umeme kupitia Airtel Money ni sehemu ya mkakati wa Airtel wa kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
Aidha ameishukuru PBZ kwa ushirikiano wake katika kuwawezesha mawakala wa Airtel Money kupata ukwasi wa kufanya miamala na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.
Naye Meneja wa Mipango na Biashara wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Aisha Omary, amesema makubaliano hayo ni mwanzo mzuri wa kupanua huduma za ununuzi wa umeme na kuwapa wateja chaguo zaidi katika kupata huduma hiyo muhimu.
Amesema umeme si anasa bali ni huduma muhimu kwa maendeleo ya wananchi, hivyo ZECO inaendelea kutafuta njia mbalimbali za kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi kwa urahisi na kwa wakati.
Kwa upande wake, mmoja wa mawakala wa huduma za fedha kutoka Kiembesamaki Johari Mungia amesema ujio wa Airtel Money katika huduma ya ununuzi wa umeme utarahisisha kazi za mawakala na kuongeza mzunguko wa biashara.
Aidha amesema kuwepo kwa mitandao mingi inayotoa huduma za kununua umeme kutawapa wananchi urahisi wa kupata huduma hizo karibu na maeneo yao huku mawakala wakinufaika kwa kuongezeka kwa miamala.