Zenj FM

Majaa yasiyo rasmi yawakosesha amani wakazi wa Fuoni Mnarani

12 June 2026, 15:34

Jaaa lililopo katika eneo la Fuoni Mnarani.

Na Mariamu Seif Mohd

Wananchi wa Shehia ya Fuoni Mnarani, Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, wameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la utupaji holela wa taka katika maeneo mbalimbali ya shehia hiyo, wakisema hali hiyo ni tishio kwa afya na mazingira kutokana na hatari ya kusababisha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

Wakizungumza katika kikao cha kila mwezi kinachoitishwa na Sheha wa shehia hiyo kwa ajili ya kujadili changamoto za maendeleo, wananchi wamesema mrundikano wa taka pamoja na harufu mbaya inayotokana na taka hizo umekuwa kero kubwa kwa wakazi wanaoishi karibu na maeneo yanayotumika kutupwa taka kiholela.

Akizungumzia suala hilo, Sheha wa Fuoni Mnarani, Riziki Manzil, amesema uongozi wa shehia umejipanga kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaohusika na utupaji holela wa taka.

Amesema mtu yeyote atakayebainika kufanya kitendo hicho atatozwa faini na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya dola.

Sauti ya Sheha

Naye Afisa wa Uhusiano, Habari na Elimu kutoka Manispaa ya Magharibi “B” Unguja, Khamis Said Saleh, amesema manispaa inalitambua tatizo hilo na tayari imeanza kutekeleza mikakati ya kulitatua.

 Ameeleza kuwa kampeni ya kuondoa majaa yasiyo rasmi imeanza, huku maandalizi ya kuboresha miundombinu ya ukusanyaji taka na kuongeza vifaa pamoja na magari ya kubebea taka yakiendelea.

Aidha, amesema manispaa imeandaa mpango wa kutoa elimu kwa wananchi katika shehia zote zilizopo ndani ya manispaa kuhusu usimamizi sahihi wa taka na umuhimu wa kutunza mazingira.

Sauti ya Khamis Said Saleh