Zenj FM
Zenj FM
30 July 2026, 23:13

Salhiya Salim Khatib ni Diwani wa Wadi ya Kinyasini, Wilaya ya Wete, ambaye ameonyesha kuwa vijana na wanawake wana uwezo wa kuongoza na kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya maendeleo. Kutoka kuwa mwanachama wa kawaida wa Chama Cha Mapinduzi hadi kuchaguliwa na wananchi kuwa Diwani, amejijengea sifa kwa kusikiliza wananchi na kuhamasisha ushiriki wa vijana na wanawake katika uongozi. Anaamini kuwa maendeleo ya kweli hupatikana pale jamii inaposhirikishwa kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
Na, Is-haka Mohamed Pemba
Kwa muda mrefu, vijana wengi wamekuwa wakilalamikia kukosa nafasi ya kushiriki katika vyombo vya
maamuzi yanayohusu maendeleo ya jamii zao. Wengine wameendelea kuamini kuwa sauti zao hazisikiki
kwenye vikao vya maamuzi, huku changamoto zinazowakabili zikiendelea kubaki bila ufumbuzi wa
kudumu. Lakini kwa Salhiya Salim Khatib, mwanamke kijana kutoka Wadi ya Kinyasini, Wilaya ya Wete,
hali hiyo haikuwa sababu ya kulalamika, bali ilikuwa msukumo wa kuingia katika uongozi ili kuwa
sehemu ya suluhisho.
Akiwa na umri wa miaka 33, Salhiya ni mke, mama wa mtoto mmoja na mzaliwa wa Kinyasini. Anaamini
kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kupatikana ikiwa vijana na wanawake hawatapewa nafasi ya
kushiriki kikamilifu katika kupanga na kusimamia mustakabali wa maeneo yao. Ndiyo sababu mwaka
2025 aliamua kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi na baadaye wananchi wa Wadi ya Kinyasini ili
agombee nafasi ya udiwani.
Kwa Salhiya, lengo lake kuu halikuwa kushika cheo, bali kuhakikisha vijana wanapata uwakilishi wa kweli
katika Baraza la Madiwani na kwamba changamoto zinazowakabili wanawake zinapata sauti yenye
nguvu katika vyombo vya maamuzi.
Anasema aliona kuwa kwa muda mrefu vijana wengi walikosa mtu wa kuwasemea kuhusu ajira,
ujasiriamali, mafunzo ya stadi za maisha na fursa nyingine za maendeleo. Vilevile alishuhudia wanawake
wengi wakikumbana na vikwazo mbalimbali vya kijamii vilivyotokana na mfumo wa uongozi uliotawaliwa
kwa muda mrefu na wanaume.
“Lengo langu lilikuwa kuhakikisha vijana wanapata mwakilishi anayeelewa changamoto zao na
anayepigania maslahi yao. Pia nilitaka kuona wanawake wanapata nafasi kubwa ya kushiriki katika
maamuzi na kuondokana na vikwazo vinavyowazuia kufikia maendeleo yao,” anasema Salhiya.
Safari yake ya kisiasa haikuanza kwa kugombea udiwani. Alianza kama mwanachama wa kawaida wa
Chama Cha Mapinduzi, hatua ambayo ilimpa nafasi ya kujifunza misingi ya uongozi na utumishi kwa
jamii. Baadaye alichaguliwa kuwa Katibu wa Hamasa wa Vijana katika tawi lake, kisha akawa Katibu wa
Tawi. Nafasi hizo zilimjengea uzoefu wa kufanya kazi na wananchi na kumwezesha kuelewa mahitaji ya
jamii kwa undani zaidi.
Akikumbuka hatua hizo anasema hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angekuwa Diwani, lakini alipoona
kuwa chama kinatoa nafasi sawa kwa wanachama wote, aliamua kuthubutu.
“Nilikuwa mwanachama wa kawaida ndani ya chama chetu cha CCM. Nikaona kweli chama hiki ni cha
kidemokrasia, hakina ubaguzi wala umimi. Kila mwanachama ana haki ya kushiriki na kuomba nafasi za
uongozi. Nilianza kuwa Katibu wa Hamasa wa Vijana, baadaye Katibu wa Tawi, kisha nikaomba ridhaa
ndani ya chama. Nilipopata ridhaa hiyo, nikagombea udiwani na wananchi wakaniamini. Leo
ninawahudumia kwa moyo wangu wote.”
Anaeleza kuwa ushindi wake haukuwa ushindi binafsi, bali ni ushindi wa vijana na wanawake
waliotamani kuona kizazi kipya kinapewa nafasi ya kuongoza na kuleta mawazo mapya katika
maendeleo ya Kinyasini.
Salhiya anaamini kuwa uongozi unahitaji kusikiliza wananchi, kushirikiana nao na kuwa karibu nao kila
wakati. Anasema kiongozi anayejitenga na wananchi hawezi kufahamu changamoto zao wala kutafuta
suluhisho sahihi.
Pamoja na majukumu yake ya udiwani, ameendelea kuhamasisha vijana kujitokeza katika shughuli za
maendeleo, kushiriki mikutano ya kijamii na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kupitia
taasisi za serikali na sekta binafsi.
Kwa wanawake, ana ujumbe maalumu unaolenga kuwahamasisha kuondoa hofu ya kuingia katika siasa
na nafasi za uamuzi.
“Wanawake wasiogope. Chama chetu ni cha watu wote. Vijana na wanawake watumie nguvu zao
kukitumikia chama na jamii kwa uaminifu ili kutimiza ndoto zao za uongozi. Hakuna kinachoshindikana
ukiwa na dhamira, ujasiri na kujituma.”
Safari yake isingekuwa rahisi bila sapoti ya familia. Mwenzi wake wa maisha, Kassim Abdalla Kassim,
anasema tangu mwanzo aliona ndani ya Salhiya uwezo mkubwa wa kuwa kiongozi na hakusita kumpa
moyo.
“Aliamua mwenyewe kuingia kwenye uongozi, akanieleza nia yake. Nilimwambia kama unaamini
unaweza, basi fanya. Mimi nitakuwa nyuma yako kukutia moyo. Hakurudi nyuma hata siku moja.
Alionesha ujasiri mkubwa kwa sababu ni mwanamke anayeamini katika uwezo wake.”
Kwa mujibu wa Kassim, ujasiri huo umeendelea kuonekana hata baada ya kuchaguliwa kuwa Diwani,
kwani Salhiya ni kiongozi anayesikiliza wananchi, anayefuatilia changamoto zao na kutafuta majawabu
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Anasema pia Chama Cha Mapinduzi kimemjenga kuwa kiongozi mwenye kujiamini, mwenye uwezo wa
kusimamia majukumu yake na asiyeweza kuyumbishwa na changamoto za kisiasa au kijamii.
Wananchi wa Kinyasini nao wanaeleza kuwa wameanza kuona mabadiliko katika namna viongozi
wanavyoshirikiana na vijana na wanawake. Wanasema uwepo wa Diwani kijana umewapa matumaini
mapya ya kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya wadi yao.
Salma Mohammed, mmoja wa wakazi wa Kinyasini, anasema Salhiya amekuwa mfano wa mshikamano
na ushirikiano.
“Ana ushirikiano mzuri sana na vijana wenzake katika kuzitafuta fursa za maendeleo. Hupenda kusikiliza
mawazo ya wananchi na kuwashirikisha katika shughuli mbalimbali za maendeleo.”
Kwa wengi, simulizi ya Salhiya Salim Khatib ni ushahidi kuwa uongozi haupimwi kwa umri wala jinsia,
bali hupimwa kwa maono, uadilifu na utayari wa kulitumikia taifa. Kutoka kuwa mwanachama wa
kawaida hadi kuwa Diwani wa kuchaguliwa na wananchi wa Wadi ya Kinyasini, ameonyesha kuwa ndoto
zinaweza kutimia pale mtu anapoamua kuthubutu, kuamini uwezo wake na kuwa tayari kubeba dhamana
ya kuwatumikia wengine.
Leo, Salhiya anaendelea kuandika historia yake kama mmoja wa viongozi vijana wanaoamini kuwa
maendeleo ya kweli huanza pale kila mwananchi, hasa vijana na wanawake, anapopewa nafasi ya
kushiriki katika maamuzi yanayoathiri maisha yake. Huo ndio msingi wa mageuzi anayoyapigania
Kinyasini, na urithi anaotamani kuuacha kwa vizazi vijavyo.