Zenj FM

Wazalishaji ,wafanyabiashara 300 kukutana Fahari ya Zanzibar 2026

1 September 2026, 18:38

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan.akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni.

Na Ivan Mapunda

Zaidi ya wafanyabiashara, wajasiriamali na wazalishaji 300 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026, yanayolenga kufungua fursa za masoko, uwekezaji na kuongeza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kikwajuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan, amesema maonyesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuwaunganisha wazalishaji na wafanyabiashara na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Juma amesema Fahari ya Zanzibar 2026 imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya ZEEA na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na kuwa hili litakuwa toleo la tatu tangu kuanzishwa kwa maonyesho hayo.
Amesema maonyesho hayo pia yanalenga kujenga utamaduni wa Watanzania kuthamini na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji, ajira na biashara na hatimaye kuchochea ukuaji wa uchumi.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan,

Katika kipindi cha siku 10 za maonyesho hayo, kutakuwa na siku maalumu zitakazojikita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo afya, vijana, ubunifu, utalii na sanaa, elimu ya kodi na urasimishaji wa biashara pamoja na elimu ya fedha.
Aidha, Juma amesema ZEEA kwa kushirikiana na TanTrade zitaendesha kliniki maalumu ya biashara, itakayowapa wafanyabiashara na wajasiriamali fursa ya kupata ushauri na ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika shughuli zao.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Tahir Musa, amesema ushiriki wa taasisi hiyo unatokana na jukumu lake la kisheria la kuandaa, kushiriki na kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuendeleza biashara na masoko nchini.
Amesema ZEEA na TanTrade zilitia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wakati wa Maonyesho ya 48 ya Sabasaba, ambapo moja ya maeneo ya ushirikiano ni kuhakikisha masoko yanaendelezwa, ikiwemo kupitia Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar.

Sauti ya kaimu naibu mkurugenzi mkuu wa TanTrade Tahir Musa

Naye Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa Wafanyabiashara wa Stanbic Bank, Fatma Ahmed, amesema benki hiyo imeamua kuwa mdhamini mkuu wa maonyesho hayo kwa kuchangia shilingi milioni 200, kutokana na umuhimu wake katika kukuza biashara na uchumi wa nchi.

Fatma amesema Stanbic Bank imeshiriki katika maonyesho hayo kwa lengo la kusaidia kukuza biashara na kuwawezesha wazalishaji kupata fursa za masoko pamoja na huduma za kifedha.

Sauti ya mkuu wa huduma za kibenki kwa wafanyabiashara wa Stanbic Bank,

Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026 yatafanyika kuanzia Septemba 4 hadi 14, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, yakitarajiwa kuvutia zaidi ya wageni na wanunuzi 15,000.
Maonyesho hayo yanabeba kaulimbiu “Bidhaa Zetu Ndiyo Fahari Yetu”, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuyafungua rasmi Septemba 5, 2026.