Zenj FM

Uzinduzi wa afisi ya uhamiaji Dunga waibua Wito wa kulinda utulivu wa taifa

25 April 2026, 9:01 am

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Afisi ya Uhamiaji, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra za Miaka 62 ya Muungano.

Makamu wa Rais Emmanuel Nchimbi amewahimiza wakazi wa Dunga kushirikiana na vyombo vya ulinzi kudumisha amani na utulivu nchini. Amesema ni muhimu kutoa taarifa kuhusu wahamiaji haramu na vitendo vinavyokiuka sheria ili kulinda usalama wa Taifa.

Na Mary Julius.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa wakazi wa Dunga, Mkoa wa Kusini Unguja, kuendelea kushirikiana na Idara ya Uhamiaji pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Wito huo umetolewa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Afisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kati, iliyofanyika Dunga, Zanzibar.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kuhusu wahamiaji haramu, watu wanaoishi kinyume cha sheria, pamoja na wale wanaojihusisha na vitendo vinavyokiuka masharti ya ukaazi wao. Amesema amani na umoja ni tunu za Taifa zinazopaswa kulindwa na kila Mtanzania.

Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amewasihi wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Wa Jamuhuri Ya Muungano Wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa viongozi hao wanaendelea kuchochea maendeleo ya nchi kwa kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi.

Sauti ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi,

Aidha, amezitaka taasisi za Serikali kuendelea kuwaamini wazawa kwa kuwapatia fursa za utekelezaji wa miradi ya ujenzi, hatua itakayochangia kukuza ujuzi na uwezo wa kifedha kwa Watanzania.

Ameipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji kwa kumpa mkandarasi mzawa zabuni ya ujenzi wa jengo hilo.

Makamu wa Rais ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za uhamiaji kwa kuboresha miundombinu na vitendea kazi, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kupitia mafunzo, kuboresha stahiki zao, na kufanya marekebisho ya mara kwa mara ya sheria na kanuni za uhamiaji.

Sauti ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi,

Akizungumzia historia, Makamu wa Rais amesema Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yaliyoongozwa na Abeid Amani Karume yalileta mageuzi makubwa yaliyojenga msingi wa maendeleo na kuwapa wananchi uwezo wa kujitawala.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameeleza kuwa wizara ina jukumu la kulinda mali na kuhakikisha usalama wa nchi unaimarika. Amesema jumla ya ajira 2,263 zimetolewa, zikiwemo ajira 472 Zanzibar, na juhudi zinaendelea kuboresha mifumo ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi wa huduma.

Sauti ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi.

Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Anna Peter Makakala, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.

Amesema kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2025, Bunge lilipitisha shilingi bilioni 32.7 kwa ajili ya Idara ya Uhamiaji Tanzania, ambapo miradi 47 ya maendeleo imetekelezwa katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar, shilingi bilioni 19.1 zimetengwa kwa ajili ya miradi 13, ambapo miradi tisa imekamilika kwa asilimia 100.

Sauti ya Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Anna Peter Makakala,

Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan, amesema idara hiyo imepatiwa shilingi bilioni 25.7 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo asilimia 50 zimetumika kwa shughuli za uendeshaji na asilimia 50 kwa miradi ya maendeleo.

Aidha Ameiomba Serikali kuwapatia boti kwa ajili ya doria za kuwabaini wahamiaji haramu, akisisitiza kuwa maafisa wa uhamiaji wana ujuzi wa kuendesha vyombo hivyo na kuogelea, hivyo wataweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Sauti ya Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan.