Zenj FM
Zenj FM
1 August 2026, 22:40

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limetoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Maftuh Foundation, Kibele, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii na kuonesha dhamira ya kushirikiana na jamii. Kamanda wa Polisi Mkoa huo, SACP Daniel Emmanuel Shillah, amesema msaada huo unadhihirisha upendo, mshikamano na uwajibikaji, huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limedhihirisha dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na jamii baada ya kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa Kituo cha Watoto Yatima cha Maftuh Foundation kilichopo Kibele, Wilaya ya Kati, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Daniel Emmanuel Shillah, amesema Jeshi la Polisi ni jeshi la wananchi na lina wajibu wa kuwafikia na kuwasaidia watu wote, hasa makundi yenye mahitaji maalumu.
Kamanda Shillah amesema msaada huo, ingawa ni mdogo ukilinganisha na mahitaji ya kituo hicho, umebeba ujumbe mkubwa wa upendo, mshikamano na uwajibikaji kwa jamii.
Kamanda Shillah ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia watoto hao kwa kuwa ni sehemu ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, amewahimiza watoto wanaolelewa katika kituo hicho kuendelea kuwa na maadili mema, kumcha Mwenyezi Mungu, kuwaheshimu walezi wao na kujituma katika masomo ili wawe viongozi na raia wema wa baadaye. Vilevile, amewapongeza askari walioshiriki kwa hiari kufanikisha upatikanaji wa msaada huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kusini Unguja, ACP Mohammed Abdallah Juma, amesema maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii mwaka huu yanaambatana na shughuli mbalimbali za kijamii zinazolenga kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.
Naye Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Maftuh Foundation, Fatma Ali, amesema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2017 kikiwa na watoto watano, sasa kinahudumia watoto 85.
Amesema kituo hakina mfadhili wa kudumu na kinategemea misaada kutoka kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali.
Aidha Fatma amewaomba wadau kujitokeza kusaidia ujenzi wa bweni la watoto wa kiume pamoja na kutatua changamoto nyingine zinazokikabili kituo hicho, ikiwemo uhaba wa majengo na kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali inayowaathiri watoto katika masomo na shughuli zao za kila siku.
Nao watoto wanaolelewa katika kituo hicho wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada waliowapatia na kutoa wito kwa jamii kuiga mfano huo kwa kuendelea kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu.
Maadhimisho ya Siku ya Polisi Jamii mwaka huu yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 25 Agosti mkoani Mbeya, yakihusisha shughuli mbalimbali za kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.