Zenj FM
Zenj FM
26 June 2026, 16:32

Baada ya zaidi ya mwezi mmoja wa kukithiri kwa taka katika eneo la Ziwatuwe, Shehia ya Amani, Manispaa ya Mjini imefanikiwa kuondoa taka hizo na kurejesha hali ya usafi. Wananchi wameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao, huku ikiahidi kuweka madampo na kuimarisha usimamizi wa taka ili kuzuia tatizo hilo kujirudia.
Na Safia na Mariamu.
Baada ya zaidi ya mwezi mmoja wa wananchi wa eneo la Ziwatuwe, Shehia ya Amani, Wilaya ya Mjini kukabiliwa na changamoto ya mrundikano wa taka, hatimaye tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi kufuatia Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Mjini kupeleka gari na kuondoa taka hizo.
Wananchi wa eneo hilo wamesema hatua hiyo imerejesha hali ya utulivu baada ya kipindi kirefu cha kukumbwa na harufu kali na ongezeko la nzi, hali iliyokuwa ikiathiri afya zao pamoja na shughuli za biashara.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao wameishukuru Serikali kwa kusikia kilio chao na kuchukua hatua ya kuondoa taka hizo.
Wamesema wafanyabiashara waliokuwa karibu na eneo hilo walipata hasara kutokana na wanunuzi kukwepa kufika eneo hilo kwa sababu ya mazingira yasiyoridhisha.
Akizungumzia suala hilo, Msimamizi wa Taka na Usafi wa Wilaya ya Mjini, Ikrima Jumanne Khamis, amesema ucheleweshaji wa kuondoa taka ulitokana na kufungwa kwa njia kwa muda wa siku 14, hali iliyositisha shughuli za ukusanyaji wa taka na kusababisha mrundikano huo.
Ameongeza kuwa baada ya zoezi la usafishaji kukamilika, Manispaa itaweka madampo mawili katika eneo hilo ili kuwezesha wananchi kuhifadhi taka kwa utaratibu, wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi wa jaa la kisasa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mjini, Dogo Iddi Mabrouk, amesema wilaya hiyo ina jumla ya majaa 59, ambapo mengi yako katika hali salama isipokuwa majaa matatu ya Ziwatuwe, Amani na Sogea yaliyokuwa na changamoto.
Aidha amesema Serikali imejipanga kuhakikisha majaa yote yanasafishwa na kuwa salama kwa matumizi ya wananchi.