Zenj FM
Zenj FM
5 July 2026, 21:00

Kambi ya mwezi mmoja ya utoaji wa miguu bandia kupitia mradi wa 100 Limb Project imewanufaisha watu 94 wenye ulemavu Zanzibar, huku wadau wakihimizwa kuendelea kuwawezesha ili wajitegemee kiuchumi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kushirikiana na taasisi zinazotoa huduma kwa watu wenye ulemavu ili kuboresha maisha yao.
Na Mary Julius.
Wadau mbalimbali wenye uwezo wametakiwa kuendelea kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa saidizi na fursa za kujikwamua kiuchumi ili kuwaondolea utegemezi na kuwawezesha kuishi maisha ya kujitegemea.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ali Omary Makame, wakati akifunga kambi ya mwezi mmoja ya utoaji wa miguu bandia iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Mbuzini kupitia mradi wa 100 Limb Project, ulionufaisha watu 94 wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Amesema viungo bandia ni vifaa vyenye gharama kubwa lakini vina mchango mkubwa katika kurejesha matumaini ya watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kutembea, kufanya kazi, kujipatia kipato na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Aidha, ameishukuru taasisi ya Naya Qadam Trust pamoja na Zanzibar Global Health Education Foundation kwa kufanikisha mradi huo, huku akiihakikishia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na kuwaunga mkono wadau wote wanaosaidia kundi hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Zariana wa Zanzibar Global Health Education Foundation, Mratibu wa Mradi wa 100 Limb Project, El Jabir Shao, ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa taasisi na watu binafsi wanaojitolea kusaidia watu wenye ulemavu.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ulihitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, hivyo amewashukuru wote waliochangia kufanikisha huduma hiyo. Pia ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Mbuzini kwa ushirikiano uliowezesha mradi huo kufanikiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Seifee Hospital Zanzibar Limited, Samuel Estomih, ameishukuru timu ya madaktari kutoka Bangladesh na Nepal pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanikisha kambi hiyo ya utoaji wa miguu bandia.
Amesema hospitali hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma maalumu za matibabu zinaendelea kuwafikia wananchi wenye uhitaji.
Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kila zinapotangazwa fursa za huduma kama hizo ili waweze kunufaika.

Nao baadhi ya wanufaika wa mradi wa 100 Limb Project wameeleza furaha na shukrani zao kwa taasisi zilizowapatia miguu bandia, wakisema sasa wataweza kurejea katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi, kujiamini zaidi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.