Zenj FM
Zenj FM
13 May 2026, 23:33

Vikundi vya VICOBA vinaendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia mfumo wa kuweka na kukopa. Zaidi ya wanachama 150 wamekutana Zanzibar kujifunza usimamizi wa vikundi, elimu ya fedha na fursa za uwekezaji kupitia kongamano hilo.
Na Mary Julius,
Uwepo wa vikundi vya VICOBA umeendelea kuchangia maendeleo ya wananchi nchini Tanzania kwa kusaidia watu wengi kujikwamua kiuchumi kupitia mfumo wa kuweka na kukopa.
Akizungumza katika kongamano la siku mbili lililofanyika Zanzibar, mwandaaji wa kongamano hilo Evance Chipindi amesema vikundi vya VICOBA vimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.
Evance amesema kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wanavicoba kuhusu usimamizi na uimarishaji wa vikundi vyao.
Aidha amewataka vijana kujiunga na vikundi vya VICOBA ili kujiajiri na kujitegemea badala ya kujiingiza katika makundi yasiyo na manufaa.
Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wajasiriamali.
Kwa upande wake Meneja Mauzo Mwandamizi wa NMB Bank, Adamu Karazani amesema benki imeshiriki katika kongamano hilo kwa lengo la kutoa elimu ya fedha na kusaidia vikundi vya VICOBA kutunza fedha zao benki kwa usalama zaidi.
Naye Mratibu wa Vikoba Unguja, Catherine Marco Ifanda amesema vicoba vimeendelea kuleta mafanikio makubwa kwa wanachama kupitia mshikamano na ushirikiano uliopo miongoni mwao.
Amesema umoja huo umewawezesha wanavikundi kusomesha watoto, kujenga nyumba pamoja na kujitegemea kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Wananzengo Vicoba Group, Scola Boniface amesema kupitia VICOBA wanachama wamefanikiwa kupata mikopo, kujenga nyumba, kusomesha watoto na kuanzisha biashara mbalimbali.
Kwa upande wake Andrea Rashid Mdesa amesema amefika Zanzibar kujifunza zaidi kuhusu uwekezaji kupitia VICOBA huku akiwashauri wanaume kujiunga katika vikundi hivyo kwa ajili ya maendeleo ya sasa na baadaye.
Kongamano hilo limewakutanisha zaidi ya wanachama 150 wa vikundi vya vicoba kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Dar es salam, Tunduma, Iringa, Arusha na wenyeji Zanzibar, ambapo baada ya kongamano washiriki watatembelea vivutio vya utalii vilivyopo Zanzibar.