Zenj FM

Watu wenye ulemavu wapigwa msasa kuifikia mikopo ya asilimia 10

3 March 2025, 4:20 pm

Mwakilishi wa Viti Maalumu kupitia nafasi za watu wenye ulemavu Mwantatu Mbarak Khamis akimkaribisha mgeni rasmi katika mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya watu wenye ulemavu visiwani Zanzibar

Na Mary Julius.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Tunu Juma Kondo, amewataka watu wenye ulemavu kufuata taratibu na vigezo vya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili waweze kufaidika.

Naibu Katibu Mkuu UWT Tunu Ameyasema haya wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya watu wenye ulemavu visiwani Zanzibar yakiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa watu wenye ulemavu mafunzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Abdulwakili, Kikwajuni Zanzibar.

Amesema watu wenye ulemavu wanakutana na changamoto katika kupata mikopo kwa sababu ya kutofuata taratibu za ujazaji wa fomu za mikopo hivyo, amewataka washiriki kuyafanyia kazi mafunzo ili lengo la kupata mikopo liweze kufikiwa.

Aidha, Tunu amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuelewa ni biashara gani wanaweza kuanzisha ili waweze kupata mikopo na hatimaye kuweza kulipa kwa wakati.

Sauti ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Tunu Juma Kondo

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Viti Maalumu kupitia nafasi za watu wenye ulemavu Mwantatu Mbarak Khamis amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajasiriamali wenye ulemavu ili waweze kufikia mikopo isiyo na riba.

Amesema wameandaa mafunzo hayo kutokana na idadi ndogo ya watu wenye ulemavu wanaojitokeza kuomba mikopo ambapo Changamoto kubwa iliyoonekana ni ukosefu wa elimu kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo.

Sauti ya Mwakilishi wa Viti Maalumu kupitia nafasi za watu wenye ulemavu Mwantatu Mbarak Khamis.

Akizungumzia mikopo kwa mtu moja moja Mkuu wa Uratibu wa Tasisi za Kifedha kutoka Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Juma Maabad Ahmed amesema utaratibu wa kupatiwa mikopo kwa mtu moja moja upo katika mchakato kwa kuandaa taratibu za upatikanaji wa mikopo.

Aidha amesema katika kurahisisha upatikanaji wa mikopo kidigital wajasiriamali wenye ulemavu wanatakiwa kuhakikisha wanavitambulisho vya mzanzibar makaazi ili iwerahisi kuingia katika mifumo hiyo.

Sauti ya Mkuu wa Uratibu wa Tasisi za Kifedha kutoka Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Juma Maabad Ahmed.
Mkuu wa Uratibu wa Tasisi za Kifedha kutoka Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Juma Maabad Ahmed katika mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya watu wenye ulemavu visiwani Zanzibar.

Wakitoa maoni yao baadhi ya wajasirimali wenye ulemavu wamesema mafunzo hayo yatawapatia muongozo katika kuzifikia fursa za mikopo.

Aidha wameushukuru Umoja wa Watu Wenye Ulemavu UWZ pamoja na wawakilishi wa viti maalum kwa kuweza kuwapatia mafunzo hayo ambayo wameahidi kuyafanyia kazi.

Sauti ya wajasirimali wenye ulemavu.

Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Wawakilishi wa Viti Maalum kupitia nafasi za watu wenye ulemavu Mwantatu Mbarak Khamis na Zainab Abdallah Salum, ambapo viongozi 60 wa vikundi vya watu wenye ulemavu wameshiriki .