Zenj FM
Zenj FM
18 July 2026, 22:53

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia uwekezaji katika miundombinu ya hospitali, vifaa tiba na huduma za uzazi salama. Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abasi Ali, amesisitiza umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki na kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza. Ziara yake katika Hospitali ya Jitimai imeambatana na kuwapongeza wahudumu wa afya pamoja na kuwafariji akina mama waliojifungua kwa kuwapatia taulo za kike.
Na Mary Julius.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeendelea kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia uwekezaji mkubwa katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na kuimarisha huduma za uzazi salama.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Siti Abasi Ali, alipowatembelea akina mama waliojifungua katika Hospitali ya Jitimai, Zanzibar, ambapo aliwapongeza kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na kuwakabidhi taulo za kike kama sehemu ya kuwafariji na kuwaunga mkono baada ya kujifungua.
Siti amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zinalenga kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuhakikisha kila mtoto anaanza maisha katika mazingira salama na yenye afya. Amesisitiza kuwa malezi bora huanza tangu mtoto anapozaliwa, hivyo amewahimiza wajawazito kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito na baada ya kujifungua ili kufuatilia afya ya mama na mtoto.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza, akieleza kuwa hatua hiyo huimarisha afya ya mtoto, huchochea ukuaji bora na kuongeza kinga dhidi ya magonjwa.
Aidha Mkurugenzi siti amepongeza uongozi na watumishi wa Hospitali ya Jitimai kwa kujituma na kutoa huduma kwa weledi, akisema mchango wao unaendelea kuokoa maisha ya akina mama na watoto.
Kwa upande wake, Daktari Dhamana wa Hospitali ya Jitimai, Dkt. Shabbier Adamjee, amesema hospitali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya wakati wote. Ameongeza kuwa ziara ya Mkurugenzi ni ishara ya uongozi unaowajali wananchi pamoja na watumishi wa sekta ya afya.
Naye Afisa Muuguzi wa Wodi ya Wazazi, Khadija Rajabu Khatibu, amesema hospitali inaendelea kutoa huduma bora za afya ya mama na mtoto, jambo lililosababisha kupokea wagonjwa wengi kutoka wilaya mbalimbali za Zanzibar.
Ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kuboresha miundombinu, vifaa tiba na mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya.
Nao Baadhi ya akina mama waliojifungua katika hospitali hiyo wameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kuboresha huduma za afya ya uzazi. Wamesema huduma wanazopatiwa na madaktari pamoja na wauguzi ni za kiwango cha juu, zimewapa faraja na kuwawezesha kujifungua salama.