Zenj FM

Dimani yapanga operesheni maalumu kudhibiti matumizi na biashara ya madawa ya kulevya

21 June 2026, 20:32

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani kichama, Rehema Makame Msheli,akiwa na baadhi ya wajumbe wa wilaya ya Dimani kichama katika kikao cha Kamati ya Kikanuni na Kikatiba kinachofanyika kila baada ya miezi sita kwa lengo la kujadili changamoto za wananchi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani Kichama, Rehema Makame Msheli, amewataka wazazi kuimarisha malezi ya watoto ili kuwakinga dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya. Viongozi wa wilaya hiyo wameeleza kuwa matumizi ya madawa ya kulevya yanachangia ongezeko la uhalifu na kuhatarisha usalama wa wananchi, hivyo wamepanga kufanya operesheni maalumu za kuyadhibiti.

Na Mariamu na Safia

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani kichama, Rehema Makame Msheli, amewataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuwapatia watoto wao malezi bora ili kuwakinga dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Ameyasema hayo katika kikao cha Kamati ya Kikanuni na Kikatiba kinachofanyika kila baada ya miezi sita kwa lengo la kujadili changamoto za wananchi, zilizopatiwa ufumbuzi pamoja na zile ambazo bado hazijatatuliwa. Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Dimani.

Rehema amesema kikao hicho kimeitishwa mahsusi kujadili namna ya kukabiliana na changamoto ya matumizi ya madawa ya kulevya, akieleza kuwa asilimia kubwa ya watumiaji wa madawa hayo hujihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, ubakaji, mauaji pamoja na matatizo ya afya ya akili.

Sauti ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani kichama, Rehema Makame Msheli.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Dimani, Khatib Mjaka Hamadi, amesema ongezeko la watumiaji wa madawa ya kulevya linaathiri amani na usalama wa wananchi, kwani wengi wao wanaishi kwa hofu ya kupoteza maisha na mali zao.

Kutokana na hali hiyo, amesema wameamua kuweka siku maalumu za kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti na kutokomeza matumizi na biashara ya madawa ya kulevya.

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gharib Muhammed Adil, amesema wataendelea kushirikiana na jamii kupitia shule, maskani, sehemu za kazi na taasisi mbalimbali kwa kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Sauti ya Gharib Muhammed Adil,

Kwa upande wake  Kamishna wa Kinga, Tiba na Marekebisho ya Tabia kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Zanzibar, Juma Zidi Kheri, amesema dira ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa huru dhidi ya tatizo la madawa ya kulevya.

Ameeleza kuwa kupitia idara mbalimbali za serikali na kwa mujibu wa sheria zilizowekwa, mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu ya kinga na udhibiti wa madawa ya kulevya pamoja na kufanya mikutano ya wazi na viongozi wa jamii ili kuongeza uelewa kwa wananchi.

Sauti ya Kamishna wa Kinga, Tiba na Marekebisho ya Tabia kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Zanzibar, Juma Zidi Kheri.