Zenj FM

Siku ya wanawake yaadhimishwa kwa kufanya usafi Zanzibar

7 March 2024, 3:58 pm

Mkuu wa Wilaya ya Kati Sadifa Juma Khamis  akifanya usafi katika eneo la hospital ya wilaya ya Kati.

“Endapo mwanamke atakuwa imara katika majukumu ya kila siku ataweza kuleta maendeleo makubwa katika jamii na nchi kwa ujumla”.

Na.Mary Julius

Wanawake wa Wilaya ya Kati Zanzibar wameshauriwa kuwa viongozi bora katika maeneo yao ya kazi pamoja na familia zao ili kukuza maendeleo ya nchi.

Mkuu wa wilaya ya Kati Sadifa Juma Khamis ameyasema hayo  wakati akiwa katika shughuli za usafi katika hospital ya wilaya Mwera Pongwe wilaya ya Kati ikiwa ni shamrashamra ya Siku ya Wanawake Duniani.

Aidha amesema mwanamke ni chachu ya maendeleo kisiasa, kiuchumi na kijamii endapo atawawajibika vizuri katika utendaji wa kazi zake.

Kwa upande wao Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa wilaya hiyo  wamesema udhalilishaji wa wanawake na watoto bado ni changamoto katika jamii hivyo ni vyema kuachana na tabia hizo ili kupata vizazi vilivyokuwa bora pamoja na viongozi imara wa baadaye.

Naye daktari dhamana wa hospital ya  Mwera Pongwe Mohamed Juma Nahoda amesema ni vyema umoja wa wanawake kuendeleza  maadhimisho hayo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo kama usafi wa mazingira pamoja na kuzitaka taasisi zingine kuiga mifano hiyo ili kufanikisha dhana ya maadhimisho hayo.