Zenj FM

TRA Pemba warejesha shukrani kwa walipa kodi

29 November 2023, 1:30 pm

Msaidizi Meneja huduma za Kodi TRA Mkoa wa Kikodi Pemba Nuhu Suleiman akikabidhi bati kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Michenzani Wilaya ya Mkoani Pemba  Hamou Maulif  Khamis ikiwa ni wiki ya shukran kwa mlipa kodi. Picha na Is-haka Mohammed.

Amesema wao kama wakala wa serikali wa ukusanyaji wa kodi kila mwaka wamekuwa na utaratibu wa kurejesha shukurani kwa walipa kodi ili waone kwamba kodi wanayoitoa hurudi kwao kwa njia tofauti ikiwemo hiyo ya kutoa misaada ya kijamii.

Na Is-haka Mohammed. Pemba

Katika kurejesha shukrani kwa walipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Pemba imekabidhi vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Wete na Mabati hamsini kwa ajili ya kusaidia kuendeleza ujenzi wa Bweni la wasichana katika Skuli ya Sekondari ya Michenzani Wilaya ya Mkoani.

Miongoni mwa Vifaa vilivyokabidhiwa katika hospitali huyo kwa Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali ni pamoja na mashuka, nguo za wauguzi na madaktari, pempasi kwa ajili ya wagonjwa na vifaa tiba.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Kwa niaba ya Kamishna wa TRA, Naibu huduma za ufundi Vannes Mshana amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikikusanya kodi kutoka kwa wananchi  kwa lengo la  kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake mbali ya kutoa huduma kwa wananchi.

Sauti ya Kamishna wa TRA, Naibu huduma za ufundi Vannes Mshana.

Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Kikodi Pemba Arif Moh`d Said amesema kuwa Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan na ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa mstari wa mbele kuwasogezea huduma bora wananchi, hivyo na TRA imekuwa kila mwaka ikiunga mkono juhudi za viongozi hao.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali ameushukuru uongozi wa TRA kwa kuichagua hospitali hiyo ya Wilaya ya Wete kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vina umuhimu  kwao na kuahidi kuwa  vifaa hivyo vitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Akikabidhi mabati hamsini kwa uongozi wa Skuli ya Michezani Wilaya ya Mkoani Msaidizi Meneja huduma za Kodi katika Mkoa wa Kikodi Pemba Nuhu Suleiman amesema TRA inatambua mchango katika sekta ya elimu hivyo kusaidia ujenzi huo kutaibirisha mazingira bora ya upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli hiyo Hamoud Maulid Khamis ameishukuru TRA kwa mchango wake wa bati hizo na kuuomba uongozi huo kuwa mabalozi kwa taasisi nyengine kujitokeza kuunga mkono ili kukamilisha ujenzi huo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli hiyo Hamoud Maulid Khamis.