Zenj FM

Masheha watakiwa kuyatumia maonesho ya nanenane kujiongezea elimu

10 August 2023, 2:55 pm

Mkuu wa wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis akiwa na baadhi ya masheha wilaya ya Magharib B katika maonesho ya nanenane Kizimbani Zanzibar. Picha na Khamis Said.

Amesema katika ziara yao hiyo watajifunza mbinu mbali mbali ambazo wakiitoa kwa wananchi wataweza kuisaidia kwa kiasi kikubwa wizara katika utoaji wa elimu ya kilimo na ufugaji.

Na Khamis Said

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo  Shamata Shaame Khamis amewataka masheha wa wilaya ya Magharibi B kuyatumia na kuifikisha kwa wananchi elimu ya waliyoipata katika ziara yao ya kujifunza katika maonesho ya nanenane.

Akizungumza na Masheha wa Shehia 34 za wilaya ya Magharibi B walipofanya ziara ya pamoja kutembelea maonesho ya nanenane Kizimbani, amesema masheha ndio ngazi ya chini ambayo wapo na wananchi hivyo wana wajibu wa kuwaelimisha juu ya suala ya ukulima na ufugaji wa kisasa ambao utaweza kuwapatia kipato.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis amesema lengo la ziara hiyo ni kijifunza vitu mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu.

Aidha mkuu wa wilaya Hamida amesema  katika ziara hiyo masheha na watendaji wa sekta mbalimbali wataweza kujifunza mambo mengi ikiwemo matumizi ya nishati mbadala na kuachana na matumizi ya kuni.

Nao baadhi ya masheha wamesema ziara hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuongeza uelewa wa mambo mbalimbali ambayo wataweza kuwafikishia wananchi ikiwemo utunzaji wa mazingira, kilimo na ufugaji wa kisasa ambao utawapatia kipato.