Zenj FM

Wafanyabiashara watakiwa kuhama pembezoni mwa barabara Zanzibar

18 August 2023, 3:56 pm

Mkuu wilaya ya Magharib B Hamida Mussa Khamis akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara. Picha na Khamis

Mkuu wa wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis, amewataka wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wa matunda na mbogamboga kwenda kufanya biashara zao katika masoko ya muda yaliyopangwa na serikali ikiwemo Kwerekwe C, Kwerekwe Sheli pamoja na Soko la Jumbi.

Na Khamisi

Mkuu wa wilaya ya Magharib B Hamida Mussa Khamisi amewataka wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika maeneo ya pembezoni mwa barabara ( Maeneo ya akiba ya barabara) kufuata maelekezo yanayotolewa na serikali ya kwenda kufanya biashara zao katika maeneo yaliyopangwa na kuacha maeneo hayo kwa ajili ya matumizi ya barabara.

Agizo hilo amelitoa wakati wa operasheni maalum iliyowashirikisha watendaji wa wilaya ya Magharibi B na Manispaa ya wilaya hiyo kwa lengo la kuondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo ya akiba ya barabara iliyotoka Amani hadi Kiembe Samaki jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.

Amesema maeneo ya akiba ya barabara huachwa kwa ajili ya matumizi maalum ikiwemo kupitisha huduma ya miundombinu ya maji safi pamoja na umeme hivyo mwananchi kufanya biashara ya aina yoyote katika maeneo hayo ni kwenda kinyume na sheria.

Aidha amesema kwa upande wa wafanyabiashara wa maduka yaliyopo pembezoni kwa barabara leseni zao zinaruhusu kufanya biashara ndani ya maduka yao hivyo amewasihi kuacha kuweka biashara zao katika maeneo ya akiba ya barabara.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamis

Mstahiki Meya Baraza la Manispaa ya Magharibi B Khamis Hassan Haji amesema operation hizo zitaendelea kufanywa na watendaji wa manispaa hivyo amewaomba wafanya biashara kufuata maelekezo ili kuepuka usumbufu ikiwemo kupigwa faini papo kwa papo kwa kufanya biashara katika maeneo yasioruhusiwa.

Sauti ya Mstahiki Meya Baraza la Manispaa ya Magharibi B Khamis Hassan Haji.

Zoezi hilo la kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo ya barabara lilifanyika katika barabara ya Amani hadi Kiembe Samaki na litaendelea katika barabara ya Kwerekwe hadi Fuoni.