Zenj FM

Viongozi Zanzibar watakiwa kuhamasisha ulinzi shirikishi

29 November 2023, 1:52 pm

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad akizungumza katika kongamano la siku moja lililo washirikisha, Wazazi ,walezi, Masheha wa Shehia zaidi ya 50,wanafunzi wa Skuli ,Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Maafisa wa Jeshi la Polisi. Picha na Omar Hassaan.

Jukumu la usalama wa wananchi si  la Jeshi la Polisi pekee hivyo  uwepo wa vikundi hivyo  utasaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya kihalifu katika jamii.

Na Omar Hassan.

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad amewataka  wananchi kujitolea kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuendeleza amani iliyopo  Nchini.

Amesema jukumu la usalama wa Wananchi si  la Jeshi la Polisi pekee hivyo  uwepo wa vikundi hivyo  kutasaidia kupunguza ongezeko la vitendo vya kihalifu katika jamii.

Akizungumza wakati wa akifungua kongamano la  ulinzi shirikishi huko  Ukumbi wa Skuli ya Dk Ali Muhammed Shein amesema kuwepo kwa Vikundi hivyo kutasaidia kupunguza wahalifu ndani ya  jamii.

Aidha amesema kongamano hilo litaisaidia jamii iliyoshiriki kujua lengo la kuanzishwa kwa vikundi vya polisi jamii pamoja na  kufanya kampeni ili jamii hiyo iweze kujiunga kusaidia vita dhidi ya vitendo viovu.

Aidha CP Hamad amewataka Wananchi kushirikiana na Jeshi  hilo  katika kutoa ushahidi wa kesi mbali mbali zinazojitokeza katika jamii sambamba na kuwataka kutoa taarifa mapema za udhalilishaji  ili kuweza kupatikana kwa ushahidi.

Sauti ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar CP Hamad Khamis Hamad.

Nae  Mratibu wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma Dk Ezakiel Kyogo amewataka wazazi na walezi  kuwapa watoto mafundisho waliyokuwa wakipewa zamani ili kuzuia mporomoko wa maadili katika jamii ya Zanzibar kwa maslahi ya Taifa la kesho.

Sauti ya Mratibu wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma Dk Ezakiel Kyogo

Nao  Baadhi ya washiriki katika Kongamano hilo wamelishukuru jeshi la polisi kwa kuwapaatia elimu juu ya ulinzi shirikishi Sambamba na kulitaka jeshi hilo  kuwa na programu maalumu kati ya jeshi la polisi, vikundi vya ulinzi shirikishi na wizara ya Elimu ili waweze kuzibiti vitendo vya uhalifu kati Taifa letu.

Sauti mshiriki wa kongamano

Kongamano hilo la siku moja  limewashirikisha Wazazi ,walezi, Masheha wa Shehia zaidi ya 50,wanafunzi wa Skuli mbalimbali,Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Maafisa wa Jeshi la Polisi wakijadili  umuhimu wa uwepo wa Ulinzi shirikishi katika Jamii.