Zenj FM

Awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria yazinduliwa Zanzibar

20 June 2026, 22:04

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi,Akizungumza katika uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika katika Viwanja vya Maonesho Kizimbani.

Na Berema Nassor

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na kwa ufanisi.

Akizungumza katika uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika katika Viwanja vya Maonesho Kizimbani, Rais Dkt. Mwinyi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.

Amesema kampeni hiyo imekuwa chachu ya upatikanaji wa haki kwa wananchi wengi kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria bila malipo, jambo lililosaidia kupunguza changamoto za kisheria na kuondoa vikwazo vinavyowazuia wananchi kupata haki stahiki.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa katika Awamu ya Kwanza ya kampeni hiyo, iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, zaidi ya wananchi milioni nne walinufaika na huduma za msaada wa kisheria katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar.

Aidha, ametoa wito kwa taasisi zote zinazohusika na utoaji wa haki pamoja na wadau mbalimbali kuimarisha ushirikiano ili Awamu ya Pili ya kampeni hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni na makundi yenye mahitaji maalumu.

Sauti Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi.