Zenj FM
Zenj FM
11 June 2026, 14:47

Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, amesema watoto milioni 138 duniani wanajihusisha na ajira za watoto, huku milioni 54 wakifanya kazi hatarishi. Amesema Zanzibar asilimia 7.5 ya watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 17 wanahusika katika ajira za watoto kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024.
Na Mary Julius.
Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif, amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) na UNICEF za mwaka 2024, watoto milioni 138 duniani wanajihusisha na ajira za watoto, huku milioni 54 wakifanya kazi hatarishi zinazohatarisha afya, usalama na maendeleo yao.
Waziri Sharif ametoa taarifa hiyo leo katika ukumbi wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji uliopo Mwanakwerekwe, Wilaya ya Magharibi B, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Dunia ya Kupinga Ajira za Watoto.
Amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar, takwimu za mwaka 2024 zinaonesha asilimia 7.6 ya watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 17 wanafanya kazi, asilimia 7.5 wako katika ajira za watoto na asilimia 7.4 wanajihusisha na kazi hatarishi.
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ajira za watoto kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha nambari maalum ya simu 0650 020296 kwa ajili ya kupokea taarifa na malalamiko ya ajira za watoto, ambapo hadi sasa taarifa 15 zimepokelewa.
Aidha, amesema Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani imeandaa Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ajira za Watoto wa mwaka 2026 hadi 2032, ambao umeanza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.
Waziri Sharif pia ameeleza kuwa kupitia Dawati la Kupinga Ajira za Watoto lililopo Bandari ya Malindi, watoto 2,340 waliingia Zanzibar kati ya Julai 2025 na Machi 2026, ambapo watoto 1,467 walibainika kuingia kwa lengo la kufanya kazi.
Akizungumzia sababu zinazopelekea ajira kwa watoto, Waziri Shariff amebainisha kuwa umaskini ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia watoto kufanyishwa kazi.
Aidha, amesema udhibiti wa watoto kutoka kwa wazazi na walezi ni muhimu, kwani wakati mwingine mzazi anaweza kudhani mtoto yupo shuleni ilhali amekwenda kufanya biashara au shughuli nyingine za kujipatia kipato.
Aidha waziri Sheriff ametoa wito kwa wasimamizi wa madiko ya samaki, wavuvi, wakuu wa masoko, wakulima wa karafuu, wafanyabiashara na wamiliki wa hoteli kuacha kuwaajiri watoto, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaokiuka sheria hiyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Kadi Nyekundu kwa Ajira za Watoto: Haki na Ulinzi kwa Watoto, Kazi zenye Staha kwa Watu Wazima.”