Zenj FM
Zenj FM
11 August 2026, 13:46

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza umuhimu wa usajili wa matukio muhimu ya maisha, huku ikisogeza huduma hizo karibu na wananchi wa Tumbatu. Wananchi wamepatiwa huduma za usajili wa vizazi na vifo, vyeti vya kuzaliwa pamoja na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Na Mwandishi wetu.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema usajili wa matukio muhimu ya maisha ni msingi wa utambulisho wa kisheria na mipango ya maendeleo ya nchi.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, ZCSRA, Makame Mussa Mwadini, amesema hayo Tumbatu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usajili Barani Afrika.
Makame amesema usajili wa vizazi, vifo, ndoa na talaka kwa wakati una umuhimu si kwa mwananchi pekee, bali pia kwa Serikali katika kupata takwimu sahihi za kupanga huduma za afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema Serikali imeendelea kusogeza huduma hizo karibu na wananchi, kutumia mifumo ya kidijitali na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Katika maadhimisho hayo, wananchi wa Tumbatu wamepatiwa huduma za usajili wa vizazi na vifo, vyeti vya kuzaliwa pamoja na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Haji Abdalla Ali, mkazi wa Tumbatu Gomani, amesema kusogezwa kwa huduma hizo kumewapunguzia wananchi usumbufu wa kusafiri kwenda maeneo ya mbali.
Aidha ameiomba Serikali kuendelea na utaratibu huo mara kwa mara ili wananchi waendelee kupata huduma kwa urahisi.
Kwa upande wake, Tatu Khamis Makame, mkazi wa Tumbatu Kichangani, amesema amefika katika zoezi hilo na kufanikiwa kupata Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi baada ya awali kushindwa kupata huduma hiyo.