Zenj FM
Zenj FM
13 June 2026, 22:10

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na SOS Children’s Village imetoa mafunzo ya ulinzi na hifadhi ya mtoto kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto. Mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa na uwezo wa askari katika kuzuia, kuchunguza na kushughulikia kwa weledi matukio ya udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto
Na Omary Hassan.
Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na SOS Children’s Village imeendesha mafunzo ya ulinzi na hifadhi ya mtoto kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Uendeshaji wa Wizara hiyo, Juma Ali Simai, amesema elimu ya kupinga ukatili kwa watoto ni miongoni mwa mikakati muhimu ya Serikali katika kuhakikisha watoto wanalelewa na kuishi katika mazingira salama yanayoheshimu haki zao.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Hifadhi ya Mtoto kutoka Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii, Mkasi Abdulla Rajab, amesema mafunzo hayo yamelenga vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na nafasi yao muhimu katika kuzuia, kufuatilia na kushughulikia makosa ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto.
Kwa upande wake, Afisa Mradi wa Kuimarisha Familia kutoka SOS Children’s Village, Khadija Issa Masoud, amesema taasisi hiyo imefadhili mafunzo hayo kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda ustawi wa watoto na kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Kamisheni ya Polisi Zanzibar, ASP Ali Mohamed Othman, amesema mafunzo hayo yatawaongezea askari uwezo na uelewa wa kushughulikia kwa weledi na kwa kuzingatia maslahi ya mtoto kesi zinazohusiana na ukatili wa kijinsia na aina nyingine za udhalilishaji.