Zenj FM
Zenj FM
7 June 2026, 22:08

Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya sheria yataongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi. Mahakama ya Zanzibar imezindua mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri unaotarajiwa kuanza kutumika kikamilifu katika mahakama zote kuanzia mwezi Julai.
Na Mary Julius.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya sheria ni hatua muhimu ya kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi.
Akifungua Mkutano Mkuu wa 26 wa Zanzibar Law Society uliofanyika katika hotel ya Golden Tulip Zanzibar Airport, Rais Mwinyi amesema teknolojia inaweza kusaidia kupunguza ucheleweshaji wa mashauri, gharama za huduma za kisheria na kurahisisha wananchi kupata haki kwa wakati, hususan wale wanaoishi maeneo ya mbali.
Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali mahakamani ili kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa na kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdallah amepongeza juhudi za Rais Mwinyi katika kuimarisha sekta ya sheria, akieleza kuwa hatua mbalimbali zilizochukuliwa zimechangia kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma za haki nchini. Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni ujenzi wa mahakama za kisasa pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi wa taaluma ya uwakili kupitia Kamati ya Nidhamu na Maadili ya Mawakili.
Jaji Mkuu amesema Mahakama ya Zanzibar tayari imezindua mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa mashauri na kwamba maandalizi yanaendelea kuhakikisha matumizi kamili ya mfumo huo yanaanza katika mahakama zote Zanzibar kuanzia mwezi Julai.
Naye Rais wa Zanzibar Law Society, Joseph Magazi, amesema kaulimbiu ya mkutano huo inalenga kuimarisha utoaji wa haki unaokwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia. Ameeleza kuwa chama hicho kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuajiri Afisa Mtendaji Mkuu na kutambulika rasmi kwa mawakili kupitia mfumo wa namba maalumu za utambulisho wa kitaaluma.
Akitoa mada katika mkutano huo Prof Zakayo Lukumay kutoka chuo cha sheria amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika utoaji wa haki yatachangia kupunguza mrundikano wa mafaili, gharama za safari na muda wa kushughulikia mashauri.
Aidha amehimiza ushirikishwaji wa wananchi katika mjadala wa haki za kidijitali ili kuhakikisha huduma za haki zinapatikana kwa urahisi, usawa na gharama nafuu kwa makundi yote ya jamii.
Kauli Mbiu: Katika Mkutano Huo Ni Kukumbatia Mageuzi Ya Kidigital Kwa Haki Bora Na Inayo Fikika Zanzibar.