Zenj FM
Zenj FM
30 July 2026, 21:50

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Galos Nyimbo, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi, wahudumu wa afya na jamii ni muhimu katika kupunguza vifo vya mama na mtoto vinavyoendelea kuathiri mkoa huo. Serikali imeendelea kuwekeza katika hospitali, vituo vya afya, vifaa tiba na rasilimali watu, huku ikisisitiza utoaji wa huduma bora, zenye utu na uwajibikaji. Wataalamu wa afya wameeleza kuwa kuchelewa kuanza kliniki, upungufu wa damu, shinikizo la damu wakati wa ujauzito na kuchelewa kufika hospitalini ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia vifo hivyo.
Na Mary Julius,
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Galos Nyimbo, amesema ushirikiano kati ya viongozi wa serikali, wahudumu wa afya na jamii ni muhimu katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyoendelea kuathiri mkoa huo.
Amesema afya ni jukumu la kila mmoja na si la Wizara ya Afya pekee, hivyo amewataka viongozi wa wilaya, masheha na wahudumu wa afya kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati.
Akizungumza katika mkutano wa kuimarisha ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto uliofanyika Bubwini, Misufini Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkuu wa Mkoa Nyimbo amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, vifaa tiba pamoja na rasilimali watu.
Aidhaa amesema uwekezaji huo unapaswa kuendana na utoaji wa huduma zenye utu, huruma na uwajibikaji kwa wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema dira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya afya ni kuhakikisha ubora wa huduma unakuwa kipaumbele cha kwanza ili kuwa na wananchi wenye afya bora.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha sekta hiyo kwa kujenga hospitali za mikoa na wilaya, kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuongeza rasilimali watu.
Dkt. Mngereza amesema ubora wa huduma za afya haupimwi kwa majengo na vifaa pekee, bali pia namna watumishi wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya kazi.
Naye Meneja wa Kitengo Shirikishi Afya ya Uzazi na Mtoto, Dkt. Kamilya Ali Omary, amesema Mkoa wa Kaskazini Unguja bado unakabiliwa na kiwango cha juu cha vifo vya mama na mtoto.
Aidha amezitaja sababu zinazoendelea kuchangia hali hiyo kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa wajawazito kuanza kliniki, upungufu wa damu, shinikizo la damu wakati wa ujauzito pamoja na kuchelewa kufika hospitalini wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu wa PharmAccess Zanzibar, Dkt. Faiza Bwanakheir Abass, amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kutumia mifumo ya kidijitali katika kufuatilia ubora wa huduma za afya.
Amesema mifumo hiyo inasaidia kubaini changamoto zinazojitokeza katika vituo vya afya, kufuatilia huduma zinazotolewa kwa wajawazito na kusaidia viongozi kufanya maamuzi sahihi katika kuboresha huduma.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Kusimamia Viwango na Ubora Hafsa Haji amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha vituo vyote vya afya vinapata ithibati ya ubora wa huduma.
Aidha amezitaja baadhi ya changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi kuwa ni pamoja na ukosefu wa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi, udhaifu wa uongozi na matumizi hafifu ya takwimu katika kufanya maamuzi.