Zenj FM
Zenj FM
12 September 2026, 15:14

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali inaendelea kuwawezesha wananchi wa Kijini kupitia mitaji, mafunzo na miradi mbalimbali ya maendeleo. Amewataka wananchi kutumia fursa za michezo kukuza afya na vipaji, huku wawekezaji wakitoa ajira kwa vijana wenye sifa. Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa na kuhakikisha mitaro na mazingira yao yanakuwa safi.
Na Mary Julius.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia miradi na programu mbalimbali za maendeleo.
Hemed amesema hayo katika uzinduzi wa Bonanza la Kijini Shangwe 2026, lililofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Kijini, Wilaya ya Kaskazini “A”, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema bonanza hilo limelenga kuwaunganisha wananchi wa Jimbo la Kijini na kuhamasisha maendeleo,
Makamu amesema jimbo hilo linaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ikiwemo miundombinu ya shule, maji safi na salama, barabara pamoja na uwanja wa mpira.
Amesema wanawake wamekuwa wakipatiwa mitaji kupitia vikundi mbalimbali, huku vijana wakipatiwa mafunzo ya umeme, welding, ufundi bomba na useremala, hatua inayowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Aidha, amewataka wawekezaji, hususan katika sekta ya hoteli na miradi mbalimbali iliyopo Kijini na maeneo jirani, kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wenye sifa kutoka maeneo hayo.
Sambamba na hayo, Hemed amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za Vuli zinazotarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba 2026, ambazo zinatarajiwa kuambatana na athari za El-Nino na kusababisha mvua kubwa, hasa katika miezi ya Novemba na Disemba.
Ametoa wito kwa wananchi kufanya usafi wa mazingira, kusafisha mitaro, kutotupa taka kwenye njia za maji na kuhama maeneo hatarishi, hususan maeneo ya vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RISE AND RESTORE FOUNDATION, ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kijini na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Badria Atai Massoud, amesema taasisi hiyo inalenga kuwawezesha wanawake na vijana kupitia mitaji, ujuzi na fursa za ajira.
Badria amesema viongozi wa Jimbo la Kijini pia wamejikita katika kuimarisha elimu kwa kuweka mazingira bora ya kusomea na kujifunzia ili kuongeza ufaulu.
Aidha Amewashukuru wafadhili na wahisani walioshiriki kufanikisha Bonanza la Kijini Shangwe kwa maslahi ya wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Cassian Gallos Nyimbo, amesema Mkoa huo unaendelea kukua kiuchumi na kijamii kutokana na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa.
Gallos amesema miradi hiyo imeongeza uwekezaji, kukuza sekta ya utalii na kutoa fursa za ajira kwa wananchi, huku ikiendelea kuufungua Mkoa wa Kaskazini kiuchumi.
Bonanza la Kijini Shangwe 2026 lilianza kwa matembezi na mazoezi ya viungo, na baadaye kufuatiwa na michezo mbalimbali iliyowakutanisha viongozi na wananchi wa Jimbo la Kijini.