Zenj FM
Zenj FM
29 September 2026, 19:41

Chama cha ACT Wazalendo imesema mchango wa wazee katika kujenga Zanzibar na Tanzania yenye maendeleo, umoja, upendo, amani na utulivu unapaswa kuthaminiwa na kupewa nafasi inayostahiki. Kauli hiyo imetolewa wakati Ngome ya Wazee ya chama hicho ikifanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Chake Chake Vitongoji, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi.
Na Is-haka Mohammed.
Chama cha ACT Wazalendo kimesema mchango wa Wazee katika kupatikana kwa Zanzibar na Tanzania Imara yenye maendeleo, umoja, upendo, amani, utulivu na watu wenye mshikano ni mkubwa hivyo ni vyema mchango huo kupewa thamani inayostahiki.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Ngome ya Wazee ya chama cha ACT Wazalendo Taifa Janeth Fusi alipokuwa akizungumza mara baada ya kumaliza kazi ya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya Vitongoji ikiwa ni kuelekea Sherehe za Siku ya Wazee Duniani.
Amesema pamoja na mchango wao mkubwa kwa taifa bado wazee wanakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwemo upatikanaji wa baadhi ya huduma, huku akieleza kuwepo kwa baadhi ya wazee waliolitumikia na taifa na kustaafua au kustaafishwa lakini hadi leo hawajapata stahiki zao.
Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Wilaya ya Chake Vitongoji Nassir Suleiman Hamad ameushukuru uongozi wa Ngome ya Wazee ya ACT Wazalengo kwa kufikiria jambo la kufanya usafi wa mazingira kwenye hospitali hiyo, kwani usafi katika maeneo ya hospitali ni muhimu kwa muda wote.
Naye Katibu wa Ng`ome ya Wazee Mkoa ya Mkoani Kichama ambaye pia Mwenyekiti wa Wazee katika mikoa yote minne ya Pemba Kichama Salim Abdalla Herizy amesema wanatambua kuwa usafi ndio msingi wa afya bora hivyo kufanya kwao usafi kunamaanisha kuimarisha afya ya jamii.
Chama cha ACT Kitaungana na mataifa mengine duniani kwa kufanya Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani Oktoba Mosi katika Ukumbi wa Majid Hall Unguja.