Zenj FM
Zenj FM
13 October 2026, 23:46

Wananchi wa Uzi Kiswani waeleza hofu yao kuhusu uchimbaji wa mchanga unaohatarisha usalama wa makazi na mazingira ya kisiwa hicho.
Na Mwandishi wetu
Wananchi wa Kijiji cha Uzi Kiswani, Mkoa wa Kusini Unguja, wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupiga marufuku uchimbaji wa mchanga katika fukwe za bahari, wakieleza kuwa shughuli hiyo inahatarisha makazi yao, usalama wa wananchi na mazingira ya kisiwa hicho.
Wananchi wametoa ombi hilo mbele ya Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia ACT Wazalendo, Profesa Omar Fakih Hamad, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wakazi wa kisiwa hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Omar Suleiman amesema uchimbaji wa mchanga umeongeza hofu ya maji ya bahari kuvamia makazi ya watu, huku mashimo yanayoachwa yakihatarisha usalama wa wakazi, wakiwemo watoto na wazee.
Mbali na changamoto hiyo, wananchi wameitaka Serikali kudhibiti uvuvi haramu unaoharibu matumbawe na samaki wachanga, kulinda mikoko pamoja na miti ya asili, na kuchukua hatua dhidi ya wizi na uharibifu wa mazao ya kilimo.
Aidha, wameitaka Serikali kuimarisha usimamizi wa shughuli za utalii ili zifanyike kwa kuzingatia sheria, mila na tamaduni za Wazanzibari.
Kuhusu miundombinu, wananchi wameipongeza Serikali kwa ujenzi wa barabara mpya inayounganisha kisiwa hicho, lakini wameomba kuwekwa kwa matuta ili kupunguza ajali zinazoweza kusababishwa na mwendo kasi wa waendesha pikipiki za bodaboda.
Aidha wameomba kujengwa kwa mifumo ya kupitisha maji ya bahari ili kuzuia maji kutuama na kuingia katika makazi ya wananchi, hali inayoweza kusababisha usumbufu na uharibifu wa nyumba.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Seif Hamad Suleiman, amewaahidi wananchi kuyafikisha malalamiko yao katika Baraza la Wawakilishi ili yaweze kufanyiwa kazi.
Akihitimisha ziara hiyo, Profesa Omar Fakih Hamad ameitaka Serikali kuangalia kwa karibu changamoto zinazowakabili wananchi wa Kisiwa cha Uzi, huku akiwahimiza wakazi kushirikiana katika kulinda fukwe, mikoko na rasilimali nyingine za asili kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.